Windows

SMG amtabiria makubwa Molinga



SIKU chache alizokaa na straika mpya wa Yanga, David Molinga, kocha wa timu ya vijana wa Wanajangwani hao, Said Maulid ‘SMG’, amesema mchezaji huyo akipewa muda, atafanya mambo makubwa.

SMG aliachiwa Molinga na wachezaji wengine wiki iliyopita kuwasimamia katika mazoezi, wakati Yanga ilipokuwa Botswana kuvaana na Township Rollers, ukiwa ni mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika walioshinda bao 1-0.

Akizungumza na BINGWA juzi, SMG alisema hakuna mchezaji mbovu katika kikosi cha Yanga , kinachowasumbua watu wengi ni kutokufahamu kuwa wanatakiwa kupata muda wa kutosha wa kuzoeana.

Alisema alibaki akiwafuatilia wachezaji hao, hasa wale wanaoambiwa si wazuri na kubaini viwango vyao ni bora, kinachohitajika ni muda wa kuzoeana.

“Hakuna mchezaji mbaya, tena kama hii michuano ya kimataifa ingechezwa timu zikiwa tayari zipo katika ligi, timu ingekuwa na kasi kubwa zaidi.

“Ujue mchezaji mpya unahitaji muda kidogo wa kuzoeana na wenzako uliowakuta, sasa ukiangalia timu ya Yanga, wachezaji wengi ni wapya na kila mmoja ametoka katika ligi tofauti,” alisema.

SMG alisema anaamini si Molinga pekee, bali wachezaji wengi wa Yanga watafanya vizuri na kwamba kila mmoja atafurahi kwa sababu watakuwa na mechi nyingi za ligi zitakazowajenga.

Post a Comment

0 Comments