Windows

NYUMA YA PAZIA : Akumbukwe rafiki yangu Winston Bogarde

MAISHA yanataka nini zaidi? Kimoyomoyo kila mtu atasema neno pesa. Ndiyo. Pesa. Unataka nini zaidi unapolipwa Pauni 500,000 kwa wiki. Na vipi kama unatoka nchi maskini? Utafanya nini zaidi? Kununua mitaa mitatu ya kifahari kila wiki.


Mtu mmoja akaanzisha usemi wa ‘Money makes the world go around’. Alimaanisha kwamba pesa inaifanya dunia izunguke. Ni kweli. Tunafanya kazi ili iweje? Tupate pesa. Halafu tukishapata pesa tunataka nini zaidi?


Niliwaza nilipomtazama Alexis Sanchez akitua uwanja wa ndege wa Malpensa pale Milan Jumatano mchana. Nikakumbuka kisa cha mchezaji aliyeitwa Winston Bogarde. Nikatabasamu, kisha nikacheka. Wanadamu tunatofautiana.


Nikusimulie kisa cha Bogarde. Mlinzi wa Kidachi aliyechukuliwa na Chelsea mwaka 2000 akitokea Barceolona. Alitua bure Stamford Bridge kwa sababu Barcelona iliamua kumuacha. Kocha aliyemchukua alikuwa anaitwa Gianluca Vialli.


Wakati huo anachukuliwa alikuwa na miaka 29 tu. Chelsea ikampa mkataba wa Pauni 40,000 kwa wiki. Mpaka leo hizi pesa nyingi sana. Jaribu kufikiria miaka 19 iliyopita zilikuaje? Zilikuwa nyingi zaidi. Bogarde akasaini mkataba wake wa miaka minne.


Wiki chache zilizofuata Vialli akafukuzwa. Chelsea wakamchukua kocha mwingine, Claudio Ranieri. Huyu huyu aliyeipa ubingwa Leicester City mwaka 2016. Kutua tu klabuni, Ranieri hakumpenda Bogarde. Akataka ikiwezekane aondoke kabla hata hajacheza mechi moja klabuni.​


Bodi ya Chelsea ikajaribu kumuuza lakini hakuna aliyemtaka kwa haraka haraka kwa sababu mshahara wake ulikuwa mkubwa. Bogarde mwenyewe hakutaka kuondoka. Wakajaribu kumtoa kwa mkopo bado ikashindikana.


Baadaye Bogarde akajiapiza kwamba haendi popote pale hata ikibidi asichezeshwe mechi hata moja. Bogarde akiwa na magari yake ya kifahari akawa anakula mshahara tu huku akifanya mazoezi na timu ya vijana chini ya umri wa miaka 23 pamoja na ile ya wachezaji wa akiba tu.


maisha yanataka nini zaidi ya pesa? Bogarde akawa anaenda mazoezini na magari yake ya kifahari tofauti. Leo Ferrari, kesho Lamborghini, keshokutwa Range Rover. Anapishana na wachezaji wa timu ya wakubwa anatabasamu tu. Maisha yanataka nini zaidi? Wenzake wanahenyeka kweli kweli kupata pesa zao, yeye anazipata kwa ajili ya mazoezi tu.


Mkataba ulikuwa unawabana Chelsea. Walikuwa hawapumui lakini hawana cha kumfanya Bogarde. Alicheza mechi 11 tu kwa kipindi cha miaka minne Stamford Bridge. Zilikuwa mechi ndogo ndogo za michuano mbalimbali na nyingi kati ya hizo zilikuwa za michuano midogo. Alikuwa anakula mshahara mkubwa kuliko wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza.


Maisha yanataka nini zaidi? Bogarde alichukuwa ubingwa wa Ulaya na Ajax mwaka 1995. Alikuwa ametwaa mataji mbalimbali na Ajax. Alikuwa ametwaa La Liga na Barcelona mara mbili, mwaka 1998 na 1999. Lakini pia alikuwa ametwaa mataji mengine na Barcelona.


Zaidi ya yote, Bogarde alikuwa amejumuishwa katika vikosi vya michuano ya Euro 96 nchini England pamoja na Kombe la Dunia mwaka 1998 nchini Ufaransa. Hakucheza lakini alijihesabia kwamba na yeye ameshiriki michuano mikubwa kama hiyo.


Alichoona kuwa amebakiza ni pesa tu. Kuona hivyo waandishi wa Kiingereza wakaanza kununa. Wakaanza kumnunia. Wakamuandika vibaya kadri walivyoweza. Wakadai kwamba ni mroho wa pesa. Wakadai ni mfano mbaya sana kwa vijana wa kileo wanaopenda pesa bila ya kufanya.


Siku moja akahojiwa akajibu “hii dunia ni suala la pesa tu, kwa hiyo unavyopewa ofa ya mamilioni inabidi uyachukue. Ni watu wachache wanaoweza kuingiza pesa nyingi. Mimi ni mmoja kati ya wenye bahati ya kufanya hivyo. Naweza kuwa mchezaji mbovu zaidi kuwahi kununuliwa katika Ligi Kuu ya England lakini wala sijali.”


Huyo ndiye Bogarde na hisia zake. Alimaliza mkataba wake na Chelsea akiwa tajiri bila ya kuchubuka uwanjani. Alipomaliza mkataba wake akaondoka zake. Mwaka mmoja uliofuata akastaafu soka. Nadhani aliwekeza pesa zake vyema. Nimemkumbuka Bogarde ninapomfikiria Sanchez. Vipi kama na yeye angeamua kufuata njia ya Bogarde? Si Sanchez tu, vipi wanasoka wengi wa kisasa wangeamua kukomalia mikataba yao minono baada ya kuchemsha klabuni muda mfupi baada ya kuwasili? Vipi na wewe unayenisoma umeunga mkono hatua ya Bogarde?


Nimemkumbuka sana Bogarde. Kila nikikumbuka stori yake huwa nacheka. Najikumbusha kwamba kumbe katika kundi la wanasoka wa kulipwa bado kuna wanasoka wenye tabia ‘za kiswahili’. Tabia za kuridhika na pesa bila ya kufanya kazi. Bahati yao kwa Manchester United. Vipi kama wangemchukua Bogarde kwa mshahara wa Pauni 500,000 kwa wiki halafu ghafla wasimhitaji kama ilivyo kwa Sanchez. Ina maana Bogarde asingeenda Inter Milan kwa mkopo na badala yake angeendelea kukomba pesa zake kama kawaida. Maisha yanataka nini zaidi? Nimemkumbuka rafiki yangu, Winston Lloyd Bogarde. Sijui yuko wapi sasa hivi. Nikimpata nitarudi tena hapa.

Post a Comment

0 Comments