Windows

Ligi Kuu ya zawadi na kukomoana -2



KATIKA toleo la jana tuliangalia mabadiliko ya kanuni za ligi yalivyoathiri kwa kiasi fulani uendeshaji wa Ligi Kuu Bara.


Endelea na pale ilipoishia...

Timu 20


Msimu wa 2004 ambao ulikuwa wa kwanza kwa Ligi ya Bara kusimama yenyewe kama Ligi Kuu ya Tanzania, ilishuhudia idadi ikipungua hadi kubaki timu 20, kutoka 24.


Timu hizi 20 ziligawanywa kwenye makundi mawili ya timu 10 kila moja huku timu nne za juu kila kundi zikifuzu kwa hatua ya nane bora, na tatu za chini zilishuka daraja.


Timu zilizoshuka zilikuwa Vijana ya Ilala Dar Es Salaam, Bandari ya Mtwara, Reli ya Morogoro, Tukuyu Stars ya Mbeya, Kariakoo ya Lindi na Pallsons ya Arusha.Mwaka huu pia, TFF lilianzishwa kuchukua nafasi ya Chama cha Soka Tanzania, FAT.




Timu 16


Msimu wa 2005, idadi ilipungua tena na kubaki timu 16.


Timu ngeni msimu huu zilikuwa Kagera Sugar ya Bukoba, Ashanti United ya Dar es Salaam na JKT Ruvu ya Pwani.


Huu ulikuwa wa kwanza ligi kuchezwa bila mfumo wa makundi. Timu za Majimaji ya Songea na Mji Mpwapwa zilishuka daraja.




KALENDA YA AGOSTI - MEI


Mwaka 2007, TFF ilibadili kalenda ya mashindano kutoka ile ya asili ya Januari - Desemba na kuwa hii ya sasa ya Agosti - Mei.


Hii ilimaanisha msimu mpya wa 2007/08 ungeanza Agosti 2007, na bingwa angepatikana Mei 2008.


Kwa bingwa asingeweza kushiriki mashindano ya Afrika kwa sababu kalenda ya CAF bado ilibaki kuwa ya Januari - Desemba.


Hivyo TFF ikaandaa mashindano maalumu kwa ajili ya kupata wawakilishi wa Tanzania kwenye Mashindano ya Afrika yatakayoanza Januari 2008.


Mashindano haya maalumu yakaitwa Ligi Ndogo.


Pia, TFF ilivunja madaraja yote, kuanzia daraja la pili hadi la nne, na kuanzisha mashindano yaliyoitwa Ligi ya taifa.


Mashindano haya yalianzia ngazi ya wilaya hadi ngazi ya taifa ndani ya msimu mmoja.


Kupitia mashindano haya, timu ingeweza kuanzishwa mwaka mmoja na mwaka huohuo ikapanda hadi Ligi Kuu.


Kupanda daraja kwa Azam FC ni matunda ya mfumo huu.




Timu 13


Ligi Ndogo ilishuhudia idadi ya timu ikipungua kutoka 16 hadi 13. Hii ni kwa sababu timu zilizoshiriki ni zile tu zilisalia Ligi Kuu kwenye msimu wa 2006.


Ligi ya 2006 ilikuwa na timu 16, timu tatu zilishuka daraja; timu hizo ni Kahama United ya Shinyanga, Bandari ya Mtwara na Transit Camp ya Dar es Salaam.


Timu 13 zilizobaki ziligawanywa katika makundi matatu; mawili yakiwa na timu 4 kila moja, na moja likiwa na timu tano.


Kila kundi lilikuwa na kituo maalumu, haikuwa nyumbani na ugenini. Timu iliyoburuza mkia katika kila kundi, katika makundi yenye timu nne, iliangukia kwenye mechi za mchujo (play off) kukwepa kushuka daraja. Kundi lenye timu tano, lilitoa timu nne kwenye mchujo wa kukwepa kushuka daraja.


AFC ya Arusha kutoka Kundi A, Polisi Dodoma kutoka Kundi B na Ruvu Shooting na Twiga Sports kutoka Kundi C ziliangukia mchujo.


Timu hizi zikacheza zenyewe kupambania nafasi mbili za kubaki Ligi Kuu. AFC ya Arusha na Ruvu Shooting, zikashuka daraja.


Polisi Dodoma na Twiga Sports ya Kinondoni Dar Es Salaam, zikanusurika.


Hata hivyo, Twiga Sports ikauza leseni yake ya Ligi Kuu kwa Pan African, kwa msimu uliofuata.


Vinara wawili wa kila kundi walifuzu kwa hatua ya pili ya ligi iliyoitwa sita bora ambayo pia ilichezwa kwa makundi katika vituo kama ilivyokuwa hatua ya kwanza.


Vinara wa kila kundi walicheza fainali. Yanga ikawa vinara wa Kundi A lililokuwa Arusha, na Simba ikawa vinara wa Kundi B lililokuwa Morogoro.


Fainali ikafanyika Morogoro na Simba kushinda kwa penati 4-3 baada ya sare ya 1-1.




Timu 14


Kalenda mpya ya Agosti - Mei ilianza kwa idadi ya timu 14, msimu wa 2007/08.


Idadi hii ilitokana na timu 11 zilizosalimika kwenye Ligi Ndogo na tatu zilizopanda daraja.


Timu zilizopanda zilikuwa Coastal Union ya Tanga, Toto Africans ya Mwanza na Manyema Rangers ya Dar es Salaam.


Baada ya msimu kumalizika, timu nne zilishuka daraja, nazo ni Ashanti United ya Dar Es Salaam. Coastal Union ya Tanga. Pan African ya Dar Es Salaam na Manyema Rangers ya Dar Es Salaam.




Timu 12


Msimu wa 2008/09 ulishuhudia Ligi Kuu ikipunguza idadi ya timu hadi kufikia 12. Hii ilitokana na kushuka timu nne katika msimu uliotangulia, na kupanda timu mbili pekee. Timu zilizopanda zilikuwa Azam FC na Villa Squad, zote za Dar Salaam.


Mwisho wa msimu, timu tatu za Polisi Morogoro, Polisi Dodoma na Villa Squad ya Dar Ea Salaam, zilishuka daraja. Idadi ya timu 12 iliendelea hadi msimu wa 2010/11.




Timu 14


Msimu wa 2011/12, idadi ya timu iliongezeka na kufikia 14.


Timu nne zilipanda daraja na kuungana na 10 zilizosalia kutoka msimu wa nyuma yake, baada ya timu mbili kushuka.


Timu zilizopanda ni JKT Oljoro FC ya Arusha. Coastal Union SC ya Tanga. Moro United ya Dar Es Salaam na FC na Villa Squad SC ya Dar Es Salaam.




Timu 16


Msimu wa 2015/16, idadi ya timu iliongezeka tena hadi kufika 16.


Timu 12 zilizosalia kutoka msimu uliotangulia baada ya mbili kushuka, ziliungana na nne zilizopanda.


Timu zilizopanda ni African Sports ya Tanga, Majimaji ya Songea - Ruvuma. Mwadui FC ya Shinyanga na Toto Africans ya Mwanza.

Post a Comment

0 Comments