Windows

ISHARA 5 HARMONIZE KUJITOA WCB

 

Kama inavyokuwa kwa mzazi na mtoto anapofikisha umri wa kujitegemea, ndivyo inavyotokea kwa staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul Kahali ‘Harmonize’ baada ya ishara tano kujitokeza zinazoashiria dalili zote za kujitoa sehemu aliyolelewa ya Wasafi Classic Baby (WCB).

 

Harmonize au Harmo ambaye alianza rasmi muziki mwaka 2015 baada ya kusainiwa na lebo hiyo iliyo chini ya staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, amekuwa akisimamiwa kazi zake za muziki ikiwemo shoo za ndani na nje ya nchi, video, kolabo za kitaifa na kimataifa na mikataba mbalimbali ambapo vyote hivyo vimemfanya kuwa msanii mwenye mafanikio ya haraka kwa sasa kwenye muziki huo.

 

TETESI ZAANZA Kwa siku za hivi karibuni taarifa zilianza kusambaa kuwa Harmo baada ya kupata mafanikio ya ndani na nje ya nchi na kuona sasa ana uwezo wa kujitegemea kwa shoo na pesa, ameanza ‘prosesi’ za kujitoa WCB taratibu.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, hata katika ufunguzi wa tamasha kubwa la Wasafi, Julai 19, mwaka huu ambalo lilianzia katika Viwanja vya Zimbihile, Muleba mkoani Kagera, Harmo hakutokea na badala yake alikuja kutokea katika tamasha hilo lilipofanyika jijini Mwanza kwa kupunguza maneno ya watu. “Anachokitaka Harmo ni kujiondoa kwa amani WCB. Anajaribu kuzima maneno yanayosambaa ili isije kuonekana kuna bifu kati yake na Mondi ndiyo maana huwezi kushangaa kumuona akipanda katika baadhi ya shoo za Wasafi,” kilianika moja ya chanzo.

 

ISHARA YA KWANZA Chanzo kingine kilianika ishara tano ambazo zimeanza kujitokeza kwa Harmo kuashiria moja kwa moja yupo mbioni kujitoa au ameshaondoka WCB.

 

Ishara ya kwanza ni kitendo cha kuonesha mabadiliko ya kuondoa utambulisho wake wa kusainiwa chini ya Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) katika ukurasa wake wa Instagram. “Ukiangalia ukurasa wake wa Instagram kwa kipindi kirefu tangu awepo katika lebo hiyo kwa upande wa juu alikuwa ameandika; ‘Signed Under WCB Wasafi’ akimaanisha amesainiwa chini ya Lebo ya Wasafi, lakini juzikati alifuta neno hilo na kuandika; ‘

 

WCB4LIFE’. “Ikumbukwe mwanzo hata msanii mwingine wa Bongo Fleva, Richard Martin ‘Rich Mavoko’ kabla ya kujitoa WCB alianza kwa kuondoa taarifa za kuwepo WCB kwenye ukurasa wake wa Instagram na baadaye
akatangaza kujitoa rasmi,” kilisema chanzo hicho.

 

ISHARA YA PILI Hii

nayo ipo ni katika ukurasa wake wa Instagram ambapo kwa muda wa miezi miwili sasa, hajaposti kazi yoyote ya bosi wake, Mondi. “Mara ya mwisho kwa Harmo kumposti au kuposti kazi ya Mondi ilikuwa ni miezi miwili na nusu iliyopita na ilikuwa baada ya kuachia Wimbo wa Inama akiwa amemshirikisha Fally Ipupa. Baada ya hapo hajawahi kuposti tena pamoja na kwamba Mondi aliachia kazi zake nyingi tu kama Kanyaga na The One. “Lakini pia Mondi naye hajawahi kuposti kazi yoyote ya Harmo kwa miezi hiyo miwili zaidi ya kuposti za wasanii wengine
kama Mbosso, Rayvanny na Romy Jones,” kilisema chanzo.

 

ISHARA YA TATU Chanzo kiliendelea kumwagika kuwa, kwa sasa Harmo ana shoo nyingi za nje ya nchi ambazo zinampa jeuri na kujiona kumbe inawezekana hata kuwa peke yake bila kusimamiwa na lebo.

 

“Kuanzia Aprili hadi Novemba, mwaka huu, amekuwa na atakuwa na shoo zaidi ya 20 za nje ya nchi, achilia mbali za ndani na zote anajaza usipime. Agosti atakuwa na shoo kubwa New York, Dallas, California na Seattle zote nchini Marekani. Oktoba atakuwa Uingereza na Australia wakati Novemba atakuwa Dubai, hapo hujataja mwezi Desemba ambao huwa na shoo nyingi zaidi kuliko miezi mingine kwa kuwa msimu wa sikukuu,” kilisema.

 

ISHARA YA NNE Kitu kingine kinacholeta ishara kuwa amejitoa au yupo mbioni kujitoa WCB ni uwepo wa lebo yake kubwa ya muziki ya Konde Gang ambayo inafanya kazi kama ilivyokuwa WCB, lakini utofauti ni kwamba inasimamiwa na Harmo.

 

“Mfumo wake ameufanya kama ilivyo kwa Mondi, anamiliki Lebo ya WCB, lakini ana mameneja wanaosaidiana naye kuiongoza ambao ni Babu Tale, Fella na Sallam. Harmo naye anamiliki Lebo ya Konde Gang anayosaidiana na meneja wake, Mjerumani (Beauty Mmari). Lebo hii ya Harmo inaongozana naye kila sehemu maalum kukava matukio na shoo zake,” kilifunguka chanzo hicho.

 

ISHARA YA TANO Kumiliki studio yake ya muziki ni miongoni mwa ishara tano za staa huyo ambapo anamiliki studio kubwa ya kutengeneza muziki iliyopo Sinza-Kijiweni jijini Dar. “Moja ya mafanikio ya Mondi ndani ya WCB ni kumiliki studio ya Wasafi Records na Harmo naye amefuata nyayo hizohizo baada ya kutumia muda mrefu kurekodi nyimbo zake Wasafi. Hii ina maana kuwa, atakuwa akifanya kazi zake bila kutegemea studio iliyomlea na kumtoa ya Wasafi,” kiliweka nukta chanzo hicho.
KAMA ANATAKA KUONDOKA, AONDOKE Alianza Mondi siku kadhaa zilizopita ambapo alikaririwa akisema; “Kama Harmonize anataka kuondoka, aondoke.” Kauli hiyo iliungwa mkono na mmoja wa mameneja wa Wasafi, Fella ambaye alisema; “Kama akiamua kuondoka, hakuna wa kumzuia.”
DIAMOND NI BABA YANGU Kwa upande wake, Harmo mwenyewe amekuwa akisisitiza kuwa hawezi kuondoka Wasafi kwani huwa anamchukulia Diamond kama baba yake kwani ndiye aliyemlea kimuziki.

The post ISHARA 5 HARMONIZE KUJITOA WCB appeared first on Global Publishers.


Post a Comment

0 Comments