Juzi Jumapili na leo Jumanne mechi zitajaa lakini haziwezi kujaa kila mechi. Kwa promosheni ya haraka haraka kama hii, uwanja unaweza kujaa kwa muda lakini kwanini uwanja hauwezi kujaa mechi ya Ndanda? Kwanini hauwezi kujaa mechi dhidi ya Alliance?
HIKI kichekesho cha kujisifu tumejaza uwanja kimetoka wapi? Nilikuwa najiuliza majuzi. Yanga waliujaza Uwanja wa Taifa katika siku yao ya kutambulisha wachezaji juzi Jumapili. Walicheza na Karobangi kutoka Kenya.
Wakaujaza kweli uwanja. Kabla ya hapo Simba walikuwa wanaujaza uwanja katika mechi nyingi za kimataifa msimu uliopita. Na hata leo Simba wataujaza Uwanja wa Taifa katika kile kinachoitwa Simba Day. Kichekesho hiki kimetoka wapi? Bado najaribu kujiuliza.
Kwanza je, kulikuwa na wasiwasi kwamba mashabiki wa Simba na Yanga hawazipendi sana timu zao? Kuna watu wamekufa kwa ajili ya hizi timu. Kuna watu wamewahi kupata ulemavu kwa ajili ya hizi timu. Kuna watu mioyo yao haijawahi kuacha kuhangaika kuhusu hizi timu. Inatokea kabla ya mechi, wakati wa mechi, na baada ya mechi. Inatokea katika maisha ya kila siku.
Pili, fanya kwamba kila timu ina mashabiki milioni tano tu kila upande. Fanya kila upande una mashabiki milioni 2 tu ndani ya Jiji la Dar es salaam. Wanashindwaje kujaza uwanja wa mashabiki 60,000? Haiwezekani. Hata kama mechi zinaonyeshwa katika televisheni.
Juzi Jumapili na leo Jumanne mechi zitajaa lakini haziwezi kujaa kila mechi. Kwa promosheni ya haraka haraka kama hii, uwanja unaweza kujaa kwa muda lakini kwanini uwanja hauwezi kujaa mechi ya Ndanda? Kwanini hauwezi kujaa mechi dhidi ya Alliance?
Sababu za watu kutokwenda uwanjani zipo wazi. Mashabiki wengi wamezichoka klabu hizi. Ulipofika mpira wa Ulaya mashabiki wakaelimika kujua jinsi timu za mpira zinavyoundwa. Wamejua mambo mengi na wamepata njia mbadala ya kuachana na mpira wetu. Zamani walikuwa wanajaa kwa sababu hawakuwa na jinsi.
Mashabiki wamejua thamani ya klabu, wachezaji na uendeshaji wa klabu zenyewe. Mashabiki wamejua mpira ni starehe. Wamejua ukienda uwanjani kama shabiki unakuwa mfalme. Unafika uwanjani, hausukumani na mtu wala kutishiwa mbwa.
Unafika uwanjani unapata bia yako kama kawaida, unakunywa mvinyo wako kama kawaida, unakula chakula kama kawaida. Unakwenda na mkeo na watoto. Hakuna tishio lolote la afya yako wala maisha yako.
Haya mambo hayapo kwetu. Haishangazi kuona mashabiki milioni mbili wa Simba au Yanga waliopo jijini Dar es salaam hawaendi uwanjani.
Kitu kingine ni kwamba kuna wachezaji wengi wa magazetini siku hizi. Ukienda uwanjani hawafikii matarajio ya mashabiki. Mashabiki wanajua thamani ya pesa zao na wana chaguo. Ama kwenda uwanjani au kutazama Manchester United na Tottenham katika televisheni. Zamani chaguo la pili halikuwepo.
Lakini hapohapo tukumbuke mashabiki zamani walikuwa wanakwenda katika mechi zote kwa sababu upinzani wa timu za mikoani na kwingineko ulikuwa mkali. Pamba ya Mwanza walikuwa Pamba haswa. Unakwenda kuwatazama kina Fumo Felician, Hamza Mponda ni kama vile umekwenda kutazama mechi ya kimataifa.
Unakwenda kuwatazama Coastal Union ya Ally Maumba na Idrissa Ngulungu inakuwa kama vile unatazama Al Ahly. Leo Coastal inafungwa mabao 8-0 na Yanga, kisha na Simba. Mashabiki waliofahamu soka la kisasa wanajua huu ni ‘wizi’ au ‘utapeli’ katika soka la kileo.
Miaka minne iliyopita Yanga na Azam FC waliukamata mpira wetu kwa upinzani wa hali ya juu na mastaa waliocheza soka la uhakika kina Thaban Kamusoko. Mechi ya Yanga na Azam ilikaribia kujaza uwanja. Kwa sababu gani? Azam walikuwa hawatabiriki.
Hata hivyo, kuna mechi kama ya juzi na hii ya leo. Kwanini mashabiki wamejaa juzi na watajaa leo? kwa sababu ya kutangaziwa mambo mengi makubwa kwa ajili ya siku moja. Lakini pia inakuwa mechi ya kimataifa. Mashabiki wanaamini timu za kigeni zinaleta mambo mengi mazuri uwanjani.
Mashabiki wengi wanajitokeza katika Uwanja wa Taifa katika mechi za kigeni kwa sababu wanaamini wapinzani ni wakali. Wanaamini wapinzani wana vitu vipya. Wanaamini wachezaji wao watapandisha viwango zaidi tofauti na wanapocheza na Ndanda.
Suala la msingi ni kwanini Simba na Yanga hazijazi uwanja mechi ya Ndanda? Kama tukifanikiwa kujaza uwanja katika pambano la ligi la kawaida dhidi ya Ndanda, ambalo halina tukio lolote kubwa, basi tutakuwa tumefanikiwa.
Vinginevyo haina maana sana kujaza uwanja mechi moja halafu wiki ijayo katika mechi ya kawaida tunarudi katika maisha ya kawaida. Hakujawahi kuwa na mjadala wa kujaza Uwanja wa Taifa. Hakujawahi kuwa na mjadala wa mapenzi ya mashabiki wa Simba na Yanga dhidi ya timu zao. Ndio maana najiuliza, mjadala huu ulianzia wapi?
Old Trafford, Emirates, Goodson Park, na kwingineko viwanja vijaa kila mwisho wa wiki bila ya kujali aina ya mechi. Crystal Palace dhidi ya Bournemouth uwanja unajaa. Sisi tunajisifu kujaza mechi moja, ushamba huu ulitokea wapi? Kuna sehemu tumekosea. Inabidi viwanja vijae kila mwisho wa wiki.
A
0 Comments