Windows

CAF yaipa Yanga kiburi


ACHANA na matokeo ya jana ambayo Yanga imepata mbele ya Ruvu Shooting pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, habari njema kwa mashabiki wa klabu hiyo ni kwamba Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limewapa jeuri mpya.


Baada ya mchezo wa jana, Yanga itaanza kujipanga kwa ajili ya kuikaribisha Zesco United inayonolewa na Mzambia, George Lwandamina ambaye aliwafundisha wababe hao wa Jangwani kwa mafanikio makubwa kabla ya Mwinyi Zahera kurithi mikoba yake.


Hata hivyo, wakati ikianza mikakati ya kusaka matokeo kwenye mchezo huo na Zesco, CAF ikawapa tumaini kwa kuwapa taarifa kuwa, wachezaji wake watatu wa kimataifa ruksa kucheza mchezo huo.


Awali, Yanga inayoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilianza kampeni zake kwa michezo miwili ya nyumbani na ugenini dhidi ya Township Rollers ya Bostwana bila kipa wake namba moja, Farouk Shikalo, beki kisiki Mustapha Seleman na straika mpya David Molinga a.k.a Falcao kutokana na kutokuwa na vibali vya CAF.


Hata hivyo, Mwanaspoti linafahamu kuwa jana Jumatano Yanga wamepewa vibali vya kuwaruhusu wachezaji hao kucheza dhidi ya Zesco United na kumpa wigo mpana Zahera kupanga kikosi kamili cha mauaji.


Mchezo wa Yanga na Zesco unatarajiwa kuchezwa kati ya Septemba 13-15, mwaka huu, ambapo baada ya mechi ya jana na Ruvu kutakuwa na mapumziko kupisha mechi za kimataifa ambapo, Tanzania itakipiga na Burundi.


Mwanaspoti lilimtafuta Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela ambaye alikiri kuwa wamepata vibali vya nyota wao wote watatu jana na limebaki jukumu la Zahera kuamua kuwatumia tu.


Alisema walipambana kuhakikisha vibali hivyo vinapatikana mapema ili kumfanya Zahera kuwa na machaguo mengi kwenye kikosi chake cha kwanza.


“Tulitumiwa ujumbe wa barua pepe (email) na CAF kwamba kufikia leo (jana)saa 8:00 mchana vibali vya wachezaji wetu wote watatu Shikhalo, Molinga na Mustapha vitakuwa vimetumwa kwetu. Tumekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na CAF kuhusiana na vibali hivyo na tunashukuru kwa sasa limekwisha,” alisema.


“Ujio wa vibali hivyo ni ishara nzuri kwa klabu kuwa haikukurupuka kufanya usajili kwa kufuata taratibu na kitu cha kumpongeza Zahera kuanza kuwapa nafasi wachezaji hao ambao tangu wamesajiliwa wamecheza michezo ya kirafiki pekee.


“Wachezaji wanatumika na wako vizuri, jana dhidi ya Ruvu wametumika na mmeona wenyewe. Kocha ameshawaandaa kimwili na kisaikolojia baada ya kukaa nje kwa muda wakisubiri vibali hivyo, kila kitu kamili sasa.”


Alipoulizwa kuhusu mchakato wa kupata katibu mkuu wa klabu baada ya nafasi hiyo kukaimiwa kwa muda mrefu, Mwakalebela alisema bado unaendelea na mambo yakiwa tayari wataweka wazi huku akibainisha kuwa nafasi ya ofisa habari iliyotangazwa juzi, mchakato wake utakamilika hivi karibuni.


“Mchakato huo utachukua wiki moja tu na Ijumaa tutafanya usaili kwa waombaji,” alisema Mwakalebela. Nafasi hiyo iliyotangazwa imemuondoa kabisa ofisa habari na kaimu katibu mkuu wa klabu hiyo kwa sasa, Dismas Ten kutokana na kukosa sifa za vipengele vilivyoainishwa ambavyo vinamtaka muombaji kuwa na elimu ya shahada ya mawasiliano ya umma na sifa za kufanya kazi ya uandishi kwa miaka mitano.


Sifa zingine ambazo muombaji anatakiwa kuwa nazo ni kufanya kazi katika gazeti la michezo na kufikia ngazi ya uhariri kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu. Ten ni mtaalamu wa masuala ya teknolojia ya mawasiliano akiwa na elimu ngazi ya cheti.


Yanga imefuzu kwa raundi ya kwanza ya Klabu Bingwa Afrika.

Post a Comment

0 Comments