KOCHA wa Simba, Patrick Aussems ameshauriwa kumtengeneza mchezaji aina ya Emmanuel Okwi, ambaye anatajwa kuwa nyuma ya mafanikio ya Meddie Kagere aliyemaliza na mabao 23 msimu uliopita.
Beki wa zamani wa timu hiyo, Frank Kasanga ‘Bwalya’ alisema Simba ina kikosi kizuri ambacho anakiamini kina uwezo wa asilimia 100 ya kutetea ubingwa wake msimu huu isipokuwa alimshauri Aussems amtengeneze Francis Kahata kuwa na usumbufu uwanjani.
Alifafanua kauli yake kuwa Okwi alikuwa mchezaji ambaye anapatikana maeneo mengi uwanjani, jambo lililomfanya Kagere kupata mpenyo wa kupiga mabao ya kutosha msimu uliopita.
“Kikosi cha Simba ni kizuri ni kutafuta namna ya kuwatengeneza baadhi ya wachezaji kuwa wasumbufu kwa malengo ya kuwapa mwanya Kagere na John Bocco kuzifumania nyavu, kocha akifanya hivyo Simba inakuwa na mvua ya mabao msimu huu.
“Nimewaona baadhi ya wachezaji wapya wana vitu miguuni, kama hawataingia katika mkumbo wa kucheza na majukwaa ya mashabiki ama starehe za Jiji la Dar es Salaam, watafanya mambo makubwa, kikubwa wafanye kile kilichowaleta kitawapa heshima pia Simba itatetea ubingwa,” alisema.
Kwa upande wa Ulimboka Mwakingwe alisema Kagere na Bocco ili waweze kuwa na mabao mengi msimu huu, alimtaka Kocha Aussemes atengeneze kombinesheni nzuri kuanzia safu ya viungo ambayo itakuwa inawalisha wafungaji mipira ya mwisho.“Unajua kila mchezaji ana uzuri wake, ndio maana unakuta watu wengi wanamkumbuka Okwi ambaye alikuwa na usumbufu ambao ulikuwa unawapa upenyo wengi kufunga mabao na ndio maana Kagere alifanikiwa sana msimu ulioisha,” alisema.
Naye Emmanuel Gabriel alisema pamoja na Simba kuwa na kikosi kizuri anachokiamini kina uwezo wa kutetea ubingwa msimu huu, anaamini wapo wachezaji kama Okwi hawakupaswa kuondolewa mapema kabla ya kupata mbadala wa kufiti majukumu yao.
“Unajua soka lina vitu vingi kuna mchezaji unaweza kumuona hana madhara uwanjani lakini ukiwauliza wapinzani ndio utajua moto ambao walikuwa wanaupata kukabiliana naye,” alisema.
0 Comments