Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amewataka waganga wakuu wa mikoa kuchukua hatua za makusudi kuzuia mbu waambukizao homa ya dengue na kusisitiza mikoa iliyo mpakani kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa ebola.
Waziri Mwalimu ameagiza hayo jana jijini Dodoma wakati akifungua mkutano kikao kazi cha viongozi mbalimbali wa hospitali za rufaa za mikoa.
Alisema waganga wakuu ambao maeneo yao yamekumbwa na ugonjwa wa homa ya dengue na hata mikoa ambayo haijakumbwa na tatizo hilo kuhakikisha wanaangamiza mazalia kwa kutumia dawa ya viuadudu.
"Ninachotaka kusisitiza kwa waganga wakuu najua wenzetu katika Wilaya na Halmashauri wanaweza wasituelewe lakini lazima tuchukue hatua za kudhibiti mbu hakuna maajabu mengine ambayo tutayafanya zaidi ya kudhibiti Mbu."
"Kwa hiyo waganga wakuu zile lita chache tunazowapa za dawa kuna wengine wanaona muda unaenda wanaenda katika mito wanazimwaga, hapana lazima tukafanye kazi ya kunyunyuzia katika mazalia ya mbu.
"Kama Wizara tumeagiza mashine mpya nane za kupulizia dawa na tutazileta katika baadhi ya mikoa ambayo ina mazalia, waganga wakuu lazima muwabane wakurugenzi lazima na wao watenge bajeti kwa ajili ya dawa na kupuliza.
Kuhusu ugonjwa wa ebola, Ummy alisema serikali inaendelea kuchukua hatua za kukabiliana na ugonjwa huo kama utatokea huku akiupongeza Mkoa wa Mwanza kwa jinsi ambavyo imekuwa ikijiandaa kama utatokea ugonjwa huo.
Kuhusu hospitali za rufaa za mikoa, Mwalimu alisema tayari mwongozo wa hospitali hiyo umekamilika na kuwa kwa kuanzia watahakikisha kila hospitali inakuwa na madakatari bingwa angalau mmoja kwa magonjwa 15.
Naibu Waziri wa ziara hiyo, Dk Faustine Ndugulile amesema hospitali za rufaa za mikoa zina wajibu wa kuendelea kuboresha huduma zake ikiwemo kuboresha huduma za afya kwa kusimamia ubora.
0 Comments