Na Mathew Kwembe, Mtwara
Timu za mikoa ya Dar es salaam na Geita zimetinga hatua ya fainali ya soka wavulana na zinatarajiwa kuchuana vikali katika mchezo mkali na wa kusisimua wa fainali utakaochezwa tarehe 3 julai, 2019 kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Mchezo huo ambao utashuhudiwa na viongozi mbalimbali wa serikali watakaoongozwa na Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo utahitimishwa na sherehe za kufunga mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA kwa mwaka 2019 katika uwanja wa Nangwanda.
Kabla ya kufanyika kwa mchezo wa fainali, kutachezwa mechi ya kutafuta mshindi wa tatu ambapo aliyekuwa bingwa mtetezi Tanga atapambana na timu ngumu ya Mwanza katika mchezo unaotarajiwa kuchezwa kuanzia saa moja asubuhi katika viwanja vya chuo cha ualimu Mtwara.
Katika michezo iliyochezwa jana, timu ya soka ya mkoa wa Dar es salaam ilifanikiwa kuingia fainali baada ya kuichapa timu ya mkoa wa Mwanza, na bingwa mtetezi Tanga alicheza na Geita katika hatua ya nusu fainali ambapo timu za Dar es salaam na Geita zilifanikiwa kusonga mbele baada ya Dar es salaam kushinda kwa 1-0, huku Geita ikiifunga Tanga kwa mikwaju ya penati 6-5 baada ya kutoka sare 1-1.
Kwa upande wa soka wasichana bingwa ni timu ya kagera amemfunga Mara magoli 3-0, mshindi wa tatu ni Kilimanjaro baada ya kumfunga mwanza 2-1,
Kwa upande wa soka maalum bingwa ni Shinyanga ambaye alimfunga Ruvuma kwa magoli 3-1, huku nafasi ya mshindi wa tatu ilichukuliwa na Mtwara baada ya kuilaza Dodoma 2-1,
Katika mchezo wa netboli bingwa wa UMISSETA 2019 ni Mwanza ambaye alimfunga Tabora, huku nafasi ya mshindi wa tatu ilichukuliwa na Tanga.
Katika fainali za mpira wa mikono zilizochezwa leo bingwa ni timu za soka za wavulana na wasichana za mkoa wa Mara baada ya kufanikiwa kuzichapa timu za wavulana na wasichana kutoka mkoa wa Morogoro.
Kwa upande wa mpira wa wavu (volleyball) bingwa ni timu ya mkoa wa Mbeya kwa wavulana ambayo iliifunga timu ya mkoa wa Mtwara, na wasichana bingwa ni Mtwara baada ya kuifunga Katavi.
Wakati huo huo tukio la ugawaji medali kwa washindi mbalimbali lilifanyika leo ambao washindi mbalimbali wa riadha mbio za mita 100, 200, 400, 800 na 1500 walipewa medali zao ambapo katika tukio hilo mikoa ya Mwanza na Mara ilitia fora kwa kujizolea medali nyingi.
Tukio la ugawaji medali pia lilishuhudiwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga.
0 Comments