Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe pamoja na Waziri wa Habari, Utalii na Mambo Kale Zanzibar,  Mahmoud Thabit Kombo na Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Ally Abeid Karume wamesaini makubaliano ya ushirikiano katika kusimamia na kutekeleza sekta za Habari, Utamaduni,Sanaa na michezo ili kuongeza tija.

Uwekaji wa saini za ushirikiano huo umefanyika leo Jijini Dodoma katika ukumbi wa chuo cha Ufundi Veta, baada ya vikao vya ngazi za wataalam na Makatibu Wakuu wa Wizara husika kuwasilisha taarifa hizo kwa Mawaziri na hatimaye kuridhia tayari kwa ajili ya utekelezaji.

“Hatua hii ni nzuri na muhimu kwetu katika kuhakikisha tunadumisha na kuhifadhi muungano wa kihistoria ambao ulioasisiwa na waasisi wa Taifa hili Mwalimu Julius Kamabarage Nyerere na Shehe Amani Abed Karume,”  Alisisitiza Dkt.  Mwakyembe.

Aidha, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo Kale Zanzibar  Mhe. Mahmoud Thabit Kombo ameeleza kuwa katika sekta ya habari ni muhimu kwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)  kushirikiana na  Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) ili kuandaa vipindi mbalimbali ikiwemo kipindi cha  utalii  Safari chaneli.

 “Kwa kutambua  umuhimu wa sekta ya utalii nchini ,  vyombo hivi vya habari TBC na ZBC vinapaswa kushirikiana kuandaa vipindi vya utalii  ili kuitangaza sekta hii nje na ndani ya nchi,” Alisisitiza Mahmoud Thabit Kombo.

Kwa upande wake Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Ally Abeid Karume  amesema kuwa katika kuhakikisha kuwa  lugha ya Kiswahili inatangazwa na kuenezwa kuna umuhimu wa kuandaa kanzi data itakayojumuisha  wataalam  wa Kiswahili ambao watakuwa wakifundisha wageni ndani na nje ya nchi.

Mawaziri hao walimalizia kwa kueleza kuwa sekta ya michezo ni sekta muhimu sana katika kutambulisha taifa kupitia michezo mbalimbali na hivyo walikubaliana   kuandaa kombe la Muungano, namna bora ya kuibua na kukuza vipaji pamoja na kuteua wajumbe wa bodi ya Baraza laTaifa la Michezo   (BMT) na Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar.