Serikali imewataka walimu kuacha kutegemea matumizi ya viboko shuleni kama njia ya kufundishia kwani inawajengea hofu na uwoga wanafunzi wa kushindwa kujiamini.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu bwana Tixon Nzunda wakati akizungumza na walimu na wanafunzi wa shule ya msingi ya ufundi ya Bukumbi iliyopo katika wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.
Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu, mwenye mamlaka ya kuchapa viboko shuleni ni mwalimu mkuu peke yake, walimu wengine hawapaswi kufanya hivyo labda kwa kibali chake.
Amesema anachukizwa sana na tabia iliyojengeka miongoni mwa baadhi ya walimu ya kudhani kuwa ili aweze kumsaidia mtoto katika elimu yake ni lazima viboko vitumike awapo shuleni.
“Kwenye psychology (saikolojia) mmesoma au kuna authority (mamlaka) inayosema unaingia darasani na fimbo? Wanafunzi wanaenda shambani upo mgongoni mwao na fimbo?” amehoji Naibu Katibu Mkuu na kuongeza:
“Kwa kuwa mmenisomea taarifa yenu ya shule na nimeona matokeo yenu ya darasa la nne na la saba ni mazuri niwasihi hebu acheni kuwachapa watoto,” amesema.
Bwana Nzunda ameongeza kuwa kama hilo watashindwa basi angalau darasani mpige marufuku hakuna mwalimu kuingia na kiboko darasani.
“Let the children be free ( acheni watoto wawe huru), build confidence ( wajengeeni watoto ujasiri) ili waweze kujiamini, kesho waje kuwa good teachers (walimu wazuri) waipende kazi ya ualimu, wengine wanaichukia kazi ya ualimu kwasababu walimu wao waliona toka wanaingia shule walimu wao ni fimbo tu, ” amesema.
Mbali na suala la viboko, Naibu Katibu Mkuu pia alizungumzia suala la kuwa na mikataba ya utendaji kazi kwa walimu.
Amesema serikali inataka kila mwalimu,kila msimamizi wa kazi ana mkataba wa utendaji kazi, lengo ni kuwapima walimu kutokana na mchango wao kwa nchi yao.
Naibu Katibu Mkuu ametaja vigezo vitatu vitakavyotumika kuwapima walimu hao kuwa ni pamoja na kuhakikisha kila mwalimu awe na mfumo wa kufundishia na kujifunzia, ambapo kila mwalimu atapaswa kuwa na azimio la kazi, mpango kazi lakini pia tunataka kuona mwalimu ana strategic plan (mpango mkakati) wa wapi anataka kuwapeleka watoto wake.
Wakati huo huo bwana Nzunda amesema kuwa serikali imetumia bilioni 29 kwa ajili ya kumalizia maboma yaliyokuwa yamejengwa na wananchi ili yakamilike na kutumika katika shule zetu.
Aidha Serikali sasa inajenga madarasa 2897 kwa shule za msingi kwa wakati mmoja na kuongeza kuwa serikali ya awamu ya tano inalenga kutumia raslimali kidogo kuleta matokeo makubwa.
0 Comments