Windows

TEWW yawakumbuka wasichana na wanawake walio nje ya Shule


Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) inaendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo wawezeshaji wa mpango wa elimu mbadala kwa wasichana na wanawake walio nje ya shule katika wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza ili kuwajengea stadi za kuwawezesha kujitambua, kutambua mazingira yao na kuchukua hatua sahihi za kujikwamua kiuchumi.

Mafunzo hayo ya siku nne yamefunguliwa rasmi na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Ndugu Godwin Barongo.

Ndugu Barongo amefafanua kuwa, mpango huo umejikita katika maeneo matatu ya kujifunza ambayo ni stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK), stadi za maisha na ujasiriamali zinazoendana na mahitaji ya jamii kwa sasa.

Aidha, ameeleza kuwa wasichana na wanawake hao watapata ujuzi wa kusindika karanga, matunda, mihogo, kutengeneza sabuni na batiki ili waweze kushiriki katika shughuli za kuwaingizia kipato hivyo kuboresha maisha yao na kuchangia katika ujenzi wa Taifa.

Ameongeza kuwa, baada ya mafunzo, wasichana na wanawake hao wataunda na kusajili vikundi vyao ili kupata mikopo ya kujiendeleza inayotolewa na Halmashauri pamoja na asasi mbalimbali zilizojikita katika kukwamua kundi hilo.

Kaimu Mkurugenzi Barongo ameeleza kuwa elimu mbadala inaweza kubadili mtizamo na fikra za jamii juu ya mtoto wa kike kwa kumwezesha kuwa mtu mwenye mchango wa thamani katika maendeleo ya jamii.

Ndugu Barongo amewataka washiriki wa warsha hii kufatilia mafunzo hayo kwa umakini kwani yataweza pia kuwaongezea ujuzi na thamani katika utendaji wao kikazi.

Mpango wa Elimu mbadala unatekelezwa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa UNESCO kwa ufadhili wa Shirika la Korea KOICA katika wilaya tatu za Sengerema, Ngorongoro na Kasulu. Mpango huu unalenga kuwafikia wasichana na wanawake 900 walio nje ya shule wenye umri kati ya miaka 14-24.

Post a Comment

0 Comments