Tanzania na Nchi ya Falme za Kiarabu (UAE) zimekubaliana kuendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kushirikiana katika masuala ya usalama wa eneo la Ghuba na bahari ya Hindi pia kusaidia kuimarisha hali ya usalama katika nchi za Somalia na Sudan.
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi katika Nchi ya Falme za Kiarabu na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu, Shehe Abdullah bin Zayed Al Nahyan.
Katika mazungumzo hayo wamekubaliana kuendelea kuimarisha udugu wa muda mrefu baina ya mataifa hayo na kufufua mazungumzo ya Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) ambayo kwa mara ya mwisho yalifanyika katika Mji wa Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu ili kuangalia fursa za kiuchumi kwa faida ya pande zote mbili.
Waziri Kabudi alisema pamoja na masuala mbalimbali waliyokubaliana, pia Shehe Al Nahyan ameahidi kufanya mazungumzo na Ubalozi wa Falme za Kiarabu uliopo nchini Tanzania ili kuharakisha matayarisho ya ubalozi huo kuhamia Dodoma baada ya serikali ya Tanzania kuupatia ubalozi huo eneo la kujenga bure.
Wakati huo huo, Waziri Kabudi amesema ziara yake nchini China imekuwa ya manufaa makubwa kiuchumi ambapo wawekezaji takribani 150 wanatarajiwa kuwasili nchini Tanzania kwa nia ya kuangalia maeneo mbalimbali ya uwekezaji.
Alisema wawekezaji hao watatanguliwa na ujumbe wa watu 10 watakaowasili mwezi huu, ikiwa ni kipindi kifupi mara baada ya Waziri Kabudi kuhudhuria mkutano wa kwanza wa maonesho ya uchumi na biashara kati ya China na Afrika uliofanyika katika mji wa Chanshang katika jimbo la Hunan, nchini China.
0 Comments