LEO Jumatatu, Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars itacheza mechi ya mwisho ya hatua ya makundi ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) dhidi ya Algeria. Michuano hiyo ambayo inafanyika Misri, ilianza Juni 21 na tamati yake Julai 19, mwaka huu.
Timu 24 zinashiriki michuano hiyo kwa mwaka huu ambapo Taifa Stars ni mojawapo ikiwa inashiriki baada ya kupita takribani miaka 39. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1980, hii ni mara ya pili. Tumeshuhudia Taifa Stars katika mechi zake mbili zilizopita dhidi ya Senegal na Kenya ikishindwa kuibuka na ushindi na kuburuza mkia hadi sasa.
Matokeo hayo yanaifanya kutokuwa na mwenendo mzuri kwenye michuano hiyo huku Watanzania wengi wakisema bado tunajifunza. Inawezekana kweli tunajifunza kutokana na kuwa na kikosi ambacho kina wachezaji wengi wanaocheza soka ndani ya nchi tofauti na wengine, lakini hilo suala la kujifunza liishie hukohuko Misri.
Tuna miaka miwili mbele kabla ya Afcon nyingine kufanyika kule Cameroon. Hiyo itakuwa 2021. Kama kweli Taifa Stars itakuwa imejifunza kitu katika michuano ya Afcon mwaka huu nchini Misri, matarajio yetu ni kuiona ikienda kushiriki tena nchini Cameroon.
Hatutarajii kuona tukikaa tena kwa takribani miaka 39 bila ya kushiriki Afcon kama ilivyokuwa sasa. Kauli ya kujifunza haitakuwa na maana kama mwaka 2021 tukishindwa kufuzu Afcon.
Hizo kauli mara nyingi zinadumaza soka letu, kikubwa ni kuwa na mikakati kabambe ya kuhakikisha soka letu linapiga hatua na kushiriki mashindano makubwa kama Afcon mara kwa mara.
The post KAMA MISRI TUMEJIFUNZA, BASI TWENDENI CAMEROON appeared first on Global Publishers.
0 Comments