Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amemsimamisha kazi Mkandarasi Kampuni ya Ndeenengo Senguo Ltd kwa kushindwa kukamilisha Mradi wa Maji wa Inchwankima-Imalabupina katika Wilaya ya Chato, mkoani Geita kwa wakati, licha ya kuahidi mbele ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kuwa angekamilisha kazi hiyo mwezi Februari, mwaka huu.
Naibu Waziri Aweso ameelekeza wakati Mkandarasi huyo amesimamishwa, Halmashauri ya Wilaya ya Chato ifanye taratibu za kuvunja mkataba na mkandarasi huyo na timu ya wataalam kutoka Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) na Geita (GEUWASA) pamoja na Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Geita washirikiane kukamilisha kazi zilizobaki na mradi uanze kufanya kazi.
Aweso amesema mkandarasi huyo hana uwezo wa kukamilisha mradi huo ambao umeanza Mei 12, 2017 na ulitarajiwa kukamilika Mei 11, 2018, akashindwa kuukamilisha pamoja na kupewa nyongeza ya muda mara mbili na sasa ameomba kwa mara ya tatu. Akisisitiza jambo hilo halivumiliki na amechukua maamuzi hayo kwa faida ya wananchi 59, 609 waishio katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato.
Wakazi wa Kijiji cha Nyamirembe wamemshukuru Naibu Waziri wa Maji kwa hatua aliyochukua kwa kuwa walishapoteza matumaini kutokana na ahadi hewa za mkandarasi huyo, wakisema uamuzi huo umewapa imani kuwa mradi huo utakamilika na kuanza kufurahia huduma ya maji wanayoisubiri kwa muda mrefu.
Utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Inchwankima-Imalabupina umefikia asilimia 80 kwa kazi ya ujenzi wa miundombinu ya maji na asilimia 100 kwa kazi ya ulazaji wa mabomba. Mradi utakapokamilika utagharimu kiasi cha Shilingi bilioni 8.3 na wakazi 59,609 katika vijiji 11 vya Nyamirembe, Kalebezo, Nyambiti, Busalala, Imalabupina, Inchwankima, Kachwamba, Idoselo, Ipandikilo, Mwangaza na Igarula watapata huduma ya majisafi na salama.
0 Comments