Mkurugenzi mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi  amefafanua kukosekana kwa mawasiliano miongoni mwa maofisa wa Uwanja wa Ndege wa O.R.Tambo kama moja ya changamoto zilizojitokeza katika ufunguzi wa safari zake kwenda Afrika Kusini.

Ijumaa iliyopita, shirika hilo lilianza kurusha ndege yake ya Airbus 220-300 kwenda Johannesburg lakini halikufanikiwa kufanya sherehe ya ufunguzi wa ruti hiyo kama ilivyokuwa imepangwa.

Taarifa za kwenye mitandao ya kijamii zilidai kuwa kutopokelewa kwa ugeni wa ATCL ni vita ya kibiashara kwa sababu ATCL sasa imekuwa ni mshindani katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.

Hata hivyo akizungumza Matindi alikana madai hayo huku akieleza kwamba hakukuwa na mawasiliano mazuri upande wa Afrika Kusini na kwamba hawakwenda nchini humo kula keki ila kuzindua ruti mpya.

Alifafanua mkasa huo kwa kuhusisha na kutopokelewa ugeni wa ATCL na mkanganyiko uliokuwepo kati ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ya Afrika Kusini (ACSA) na maofisa wa uhamiaji nchini humo.

Alisema kwamba maofisa uhamiaji hawakupewa taarifa na ACSA kuhusu ujio wa ndege ya ATCL.