Na Enock Magali,Dodoma
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa Kazi,Vijana,Ajira na watu wenye Ulemavu, Antony Mavunde amewasihi wananchi wa eneo la Mjimwema kata ya Chang'ombe jijini humo kuendelea kuwa watulivu kwani mgogoro wa ardhi unaowakabili kwa muda mrefu unaendelea kufanyiwa kazi.
Mbunge Mavunde ameyasema hayo jana wakati wa hafla ya uzinduzi wa Shina la wakereketwa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) iliyofanyika katika eneo la Soko la Chang'ombe,ambapo ameongeza kuwa katika utatuzi wa mgogoro huo hadi sasa tayari kuna hatua kadhaa zimekwisha chukuliwa tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
"Hivi sasa Mkuu wetu wa Mkoa ameunda ile kamati yake na ilirudi hapa kutoa taarifa na baadhi ya mambo yanaendelea,naomba tusubiri,tukamilishe zoezi hili,kama kutakuwa na mapungufu yatakayojitokeza kama viongozi wenu tupo tutasaidia kuweza kutatua,lakini cha msingi ni kwamba ile kero kubwa tayari hatua zimeanza kuchukuliwa"Alisema.
Kuhusu mikopo Mh.Mavunde amewaahidi wananchi na wafanyabishara wa kata hiyo kuwa,atashirikiana na viongozi wenzake ili kuwasaidia wale wote wenye vikundi kuweza kupata mikopo inayotolewa na Halmashauri ya Jiji pamoja na mifuko mingine ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.
"Sasa hivi Jiji lenu linatoa mikopo ya hadi Shilingi Milioni kumi kwa kikundi,niwaombe wafanyabiashara kama mna utaratibu wenu wa vikundi mmeuweka,niwaahidi nitashirikiana na Diwani wenu ili muweze kupata mikopo kupitia fedha hizi za Halmashauri ambapo kwa Jiji la Dodoma kwa sasa tunaongoza kwa kutoa fedha nyingi kuliko majiji yote Tanzania nzima"Aliongeza.
Aidha katika ufunguzi wa Shina hilo Mh.Mavunde pamoja na kuelezea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali katika Jiji hilo pia ameahidi kuweka uzio wa kuzuia jua katika Soko la Chang'ombe,Mipira na Jezi katika Timu ya shina pamoja na kuchangia kiasi cha Shilingi Milioni Moja kwa ajili ya kutunisha mfuko wa shina.
Wakizungumza na Muungwana Blog baadhi ya wananchi wamekiri Mbunge wao kuwa na mchango mkubwa katika kuwaletea maendeleo katika kata yao na kusema kuwa wataendelea kumpa ushirikiano na kuwa nae bega kwa bega.
0 Comments