Jumuiya ya wafanyabiashara watakiwa kutoendelea kutegemea kuuza nje bidhaa ghafi bali watumie viwanda vya nyumbani na bidhaa hizo ziongezwe thamani kwa kusindikwa na kufungashwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

Ameyasema hayo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu katika sherehe za ufunguzi wa Maonesho ya 43 ya biashara ya Kimataifa yaliyofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Wanahabari katika sherehe hizo Mh. Samia amesema kuwa jumuiya ya wafanyabiashara ina jukumu la kuwandaa wanachama wake kuwa na ufahamu wa kutosha, kuwa na uthubutu na kutayarisha miradi na kuwa tayari kupambana katika medani ya biashara.

“Ili Tanzania iweze kukidhi mahitaji ya fursa za masoko ya biashara zao, tunahitaji kufanya kazi kwa bidii kwa kuzalisha bidhaa zenye ushindani”. Amesema Mh. Samia.

Aidha, Samia amesema kuwa ili ujenzi wa Uchumi wa Viwanda ushike kasi ya kutosha, hakuna budi kwa sekta kama kama vile kilimo, mifugo,Uvuvi na madini kutoa malighafi za kutosheleza viwanda hivyo.

“Wakati tunahimiza ujenzi wa Uchumi wa Viwanda msukumo tunauweka pia kwenye sekta zinazozalisha malighafi.Sekta ya kilimo ikijipanga vema, viwanda vitapata malighafi hivyo hivyo kwa sekta ya mifugo, uvuvi, madini na sekta nyingine”. Ameongeza Mh. Samia.