Jeshi la Polisi Mkoani Pwani, limefanikiwa kuua majambazi wanne katika tukio la majibizano ya risasi baina ya polisi na majambazi hao huko eneo la Kwala , Wilaya ya Kipolisi Mlandizi.

Kamanda wa polisi mkoani hapo, Wankyo Nyigesa alisema, tukio hilo la kuuawa kwa majambazi hayo limetokea leo majira ya saa 8 mchana baada ya taarifa kulifikia Jeshi la Polisi kuwa wapo watu wamepanga kwenda kuvamia na kupora fedha ambazo zilikuwa zimepangwa kwenda kulipwa kwa wanaojenga Bandari Kavu ya Kwala.

“Ndipo Jeshi la Polisi Mkoani hapa tuliweka mtego na majambazi hao kujikuta wakinasa na kuanzisha majibizano ya risasi na kupelekea majambazi wanne kati ya sita wanaodhaniwa kuwepo kupoteza maisha,”alieleza Wankyo.

Hata hivyo majambazi wawili walitoweka eneo la tukio kwa kutumia gari lingine na msako wa kuwatafuta bado ungali ukiendelea.

Wankyo alifafanua, katika tukio hilo majambazi hao wamekutwa wakiwa na bunduki mbili aina ya pump action, radio call moja, hirizi, dawa za kupulizia watu, kamba za kufungia watu na, plasta za kuziba watu midomoni.

Vitu vingine ni pamoja na leseni za udereva, vitambulisho mbalimbali vya uraia, kadi ya bima ya afya, koti, kaniki, kanzu, suruali, kaptula.

Kamanda huyo alibainisha, miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospital ya rufaa ya mkoa ya Tumbi .