Mmoja kati ya majeruhi ambaye ni mfanyakazi wa Azam Media ya Dar es Salaam, Mohamed Mainde amesema ajali waliyoipata mkoani Singida wakati wakienda Chato, ni moja kati ya mitihani ambayo Mwenyezi Mungu, humpa kila mwanadamu kwa wakati wake.

Mainde ameyasema hayo akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) wakati Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya alipokwenda kuwapa pole wafanyakazi hao wawili, kati ya watatu waliolazwa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) jijini Arusha.

Mainde alimshukuru Manyanya kwenda kuwajulia hali na kusisitiza ajali ile ni mtihani ambao Mwenyezi Mungu humpa mwanadamu kwa wakati wake na muda husika.

"Nashukuru kwa kuja kutuona, huu ndio moyo wa upendo uliotuonesha, tumepata mtihani na leo tupo hapa na tunawashukuru madaktari kwa kutuhudumia na leo hii najisikia nafuu," alisema.

Mfanyakazi mwingine wa Azam Tv, Artus Masawe alishukuru kujuliwa hali na Naibu Waziri huyo. Alisema anajisikia nafuu baada ya kufanyiwa upasuaji wa mdomo na miguu.

Manyanya alisema tukio hilo la ajali lilipotokea, alishtuka sababu waliokufa na hao majeruhi ni watu waliojituma katika kufanya kazi bila hata kujali hadhi ya mtu.

Alisisitiza kujitoa kwao katika kazi, kuliwafanya watambulike maeneo mbalimbali. Alisema anashukuru Mungu kuwaona leo hii, wakiwa wanajitambua na wanajua wanaongea na nani.

"Nawapa pole sana na nimewapa mkono wa pole ambao utawasaidia kugharamia vitu vidogo vidogo wakiwa hapa hospitalini, nawashukuru sana madaktari kwa kutoa huduma kwa wagonjwa hawa na wagonjwa wengine, hakika Mungu ni mwema," alisema.

Mmoja kati ya madaktari aliyewafanyia upasuaji wafanyakazi hao, Dk Peter Makanza alisema Mainde amefanyiwa upasuaji mara tatu, bado operesheni mbili katika maeneo ya miguu. Jana walianza kuwafanyia mazoezi madogo wakati wiki mbili zijazo watafanyiwa upasuaji mwingine mara mbili tena.

Massawe akiendelea vyema baada ya kufanyiwa upasuaji miguuni pamoja na mdomo wake, mtaalamu wa kinywa na meno ataanza naye mazoezi ya kinywa.

Massawe anaendelea vizuri na anaongea. Juzi hospitali hiyo ilipokea majeruhi hao wawili, waliokuwa na hali mbaya. Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura, Dk Richard Mabula alisema kuwa hospitali hiyo imepokea majeruhi wawili, kati ya watatu, ambao ni wafanyazi wa Azam Media Limited.

Alisema juzi walipigiwa simu na kampuni ya ndege ya Arusha Medivac Ltd, kwa lengo la kwenda mkoani Singida katika hospitali ya wilaya, kusaidia uokoaji wa majeruhi hao watatu.

Alisema walipofika majira ya mchana Singida, waliambiwa majeruhi hao wamehamishiwa Hospitali ya Nkinga, ambapo baada ya kufika hapo, waliwachukua wakiwa katika hali mbaya, huku mmoja akiendelea kutibiwa hospitali hapo.

Alisema baada ya kuwachukua majeruhi hao, Artus Masawe (Injinia)na Mohamed Mainde (Injinia) walishauriana wawapeleke Hospitali ya Bugando Mwanza, Dar es Salaam au Arusha.

Alisema lakini rubani wa ndege hiyo(hakumtaja jina) aliona wakienda Bugando watachukua saa tatu angani na wakienda Dar es Salaam watachukua saa mbili angani ila wakija Jijini Arusha watachukua saa moja angani.

"Baada ya rubani kushauri haya tuliondoka Singida na wagonjwa hawa wawili ambao hali zao hazikuwa nzuri kisha tulitua uwanja mdogo wa Arusha saa 18:45 jioni na kuwaleta hospitalini hapa kwa ajili ya matibabu zaidi,"alieleza.

Wakati huohuo, madereva wawili waliopoteza maisha kwenye ajali iliyosababisha vifo vya wafanyakazi watano wa Azam Media, wamezikwa jana mkoani Morogoro na Tanga.

Wafanyakazi hao watano wa Azam TV waliokufa papo hapo kwenye ajali hiyo na tayari wameshazikwa ni Salim Mhando (Muongozaji wa Matangazo), Florence Ndibalema (Mhandisi wa Sauti), Sylvanus Kasongo (Mhandisi Mitambo) na wapiga picha wawili Said Haji na Charles Wandwi. Majeruhi watatu waliopona kwenye ajali hiyo, Artus Masawe, Mohammed Mwinshehe na Mohammed Mainde. Madereva waliokufa ni Omary Mhina na Juma Khatibu.