Windows

KAMA DAKIKA ZA NYONGEZA NAZO NI GUMZO, BASI HATUNA CHA KUFANYA, TUBADILIKE TUUSAIDIE MPIRA





Na Saleh Ally
MASHABIKI wa soka nchini wanaweza wakawa chanzo kikubwa sana cha kudidimia kwa mpira kama wataendelea na mfumo walionao sasa ambao unaendeshwa na "kulaumu tu."


Hakika inashangaza sana kuwaona mashabiki wa soka kila siku wakiwa wanalaumu kwa kila jambo linalotokea katika mpira na kuufanya ndio kuwa ushabiki hasa wa mpira.


Inawezekana ndani ya mpira wenyewe, mashabiki hawajui kwa nini wanashabikia na wengi wamekuwa hivyo ingawa inakuwa vigumu pia kwao kujua kama hawajitambui.


Mfano, mmoja akiwa shabiki wa Yanga anaonekana ni adui anapokuwa na mashabiki wa Simba. Au anayeishabikia Simba anapaswa kutopendwa na mashabiki wa Yanga, jambo ambalo ni ajabu sana.


Vipi watu wote wanaweza kuishabikia Yanga tu, au Simba tu! Lakini utakuwa vipi Yanga wasiwepo Simba? Utacheka na nani, utashindana na nani na nini maana ya ushabiki?


Kuna haja ya kujifunza na kujua au kujiuliza kwa nini wewe ni shabiki? Kama unapenda kufurahi na kuheshimiwa, lazima uje kwamba na wengine wanastahili kupata kama hicho chako.


Kilichonigusa hadi kuandika makala haya ni jambo la dakika, ni baada ya Simba kushinda bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania. Bao la Simba lilifungwa na Hassan Dilunga mwishoni mwa dakika saba za nyongeza.



Baada ya hapo, mitandaoni ambako kuna mashabiki wengi wajuaji, walianza kulalama, kusema maneno ya kila aina kwamba Simba walipendelewa na imekuwa kawaida yao na kadhalika.


Baada ya hapo, mashabiki wa Simba wakiongozwa na Msemaji wa Simba, Haji Manara nao wakaanza kuweka wakionyesha siku Yanga ilipovaa Lipuli FC ugenini Iringa na kufungwa kwa bao 1-0, dakika saba zilizongezwa.


Simba wakawa wakisema Yanga iliongezwa dakika saba ili isawazishe, lakini ikashindwa na mwisho ikaishia kuangukia pua. Basi mjadala ukapaa zaidi hadi watu kuanza kuzodoana, kukashifiana na kadhalika.


Mashabiki wengi wapenda mpira ambao si wazuri kupanga hoja au hawajiwezi kupanga hoja, hupenda kutukana maana matusi ni silaha ya wasiojiweza kihoja.


Basi ikawa ni kutukanana, kusemeana maneno mabaya lakini uhalisia ni kwamba jambo hilo lilianza kutokana na hoja ya kuongezwa pointi Yanga wakionekana kuzidiwa na wenzao Simba ambao waliingiza ile hoja ya Lipuli dhidi ya Yanga kuongezwa pia dakika saba.


Kweli kuna jambo la kujifunza kama sisi wapenda soka, suala la kuongezwa dakika saba linaweza kuwa jambo kubwa na gumu kiasi cha kuanza kukashifiana.


Hivi ni kweli kuongezwa dakika saba ni jambo geni katika mpira? Inasikitisha tena kuona kwamba mashabiki hawajui kuwa katika kuongezwa muda timu zote zinautumia na si timu moja peke yake inacheza kama ilivyoonyeshwa.


Maana wengi walikuwa wakilalamikia dakika kuongezwa utadhani JKT hawakuzitumia. Wengine nao wakajikita kuonyesha wenzao waliwahi kuongezewa dakika lakini wakafungwa.


Kweli hata kama ndio ushabiki, kuwa na mawazo dhaifu kama haya tunaweza kuwa chachu ya kusaidia maendeleo ya soka. Kila siku kulalamika utafikiri ushabiki bora ni ulalamikaji usioisha.


Hivi kweli kabisa timu kama Simba haiwezi kushinda hata mechi moja hadi ipendelelewe? Kuna kulalamika bao lilikuwa offside, kulalamika walitakiwa kucheza saa 8 wamecheza saa 9, kulalamika mechi yao imesogezwa mbele na sasa kulalamika hadi dakika za nyongeza ambazo zinatumiwa na timu zote mbili?



Kuna haja ya kujitathmini, naona kama tumejisahau sana. Tunakwenda na mwendo ambao utatuporomosha na hatuwezi kujifunza kwa kuwa kila kizuri cha upande mmoja kinaonekana ni upendeleo.


Kawaida maendeleo yanatokana na tamaa au hamu na hata wivu lakini uwe wa kimaendeleo. Kama mwenzako anafanya vizuri basi ni vema kumuangalia kwa jicho chanya kwa maana ya kuiga lililo bora kwa kulifanyia kazi na kuliboresha zaidi na baada ya hapo kuanza kufanya vizuri zaidi. Hii si sahihi kila zuri la upande wa pili kuonekana halifai kwa upande mwingine.


Hatuwezi kuwa wapenda mpira tunaolalamika tu kila kukicha. Wapenda mpira tusioamini wenzetu wanaweza kufanya vizuri, hii haitatusaidia na tutazidi kubaki tulipo kwa kuwa kulalamika pekee hakuwezi kuwa utatuzi wa matatizo yanayotukabiri.



Post a Comment

0 Comments