YANGA jana ilisimamisha nchi jana kutokea ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam kwenye hafla yao maalum ya kubwa kuliko. Mbali na mikakati mizito na ya maana iliyosemwa na viongozi mbalimbali waalikwa, kubwa kuliko ilikuwa utambulisho wa usajili mpya wa Yanga ambapo ukumbi mzima ulizizima.
Shangwe zilizizima jana baada ya Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela kumtambulisha straika Mganda, Juma Balinya ukumbini hapo akiambatana na Abdulaziz Makame ambae ni kiungo Mzanzibar.
Balinya ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uganda msimu huu na habari za uhakika zinadai kwamba alishamalizana na Simba na jana alikuwa aje Dar es Salaam kusaini lakini Yanga wakamnyaka juu kwa juu na kumaliza ishu.
Habari zinasema kwamba Simba walitarajia kumtambulisha Balinya jana mchana lakini mipango ikatibuka na jana amesaini miaka miwili Yanga ambapo baada ya kutambulishwa mbele ya wanachama alisisitiza kwamba anaijua Yanga na amekuja kufanya kazi.
Balinya alifunga mabao 19 akiwa na Polisi Uganda. Kituko kilichotokea kwenye usajili wa Balinya ni kwamba Simba walimleta nchini juzi saa 2 usiku lakini jana saa 7 mchana akaibukia Yanga.
Walimnyaka kimafia na kumuita chemba wakampa chake. Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla alipoulizwa alicheka na kusema;
“Alikuwa kwenye mipango yetu wala hatujampora mtu.” Majembe mengine yaliyotambulishwa jana ukumbini hapo na Mwenyekiti wa Kamati ya kuchangia Yanga, Antony Mavunde(MB) ni Mustapha Seleman, Sibomana Patrick,Abdulaziz Makame, Issa Birigimana, Maybin Kalengo, Lamine Moro na Sadney Urikhob.
Mavunde alitamba kwamba Yanga imesheheni na wachezaji hao wote na wengine watatambulishwa kwenye siku maalum ya wananchi ndani ya Uwanja wa Taifa hivikaribuni. Mavunde ambaye ni Naibu Waziri wa Kazi na Ajira alisema wamewezesha usajili wa wachezaji hao kutokana na michango mbalimbali ya wanachama na mashabiki huku akikabidhi ripoti ndefu ya mapendekezo yao kwa uongozi.
Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla yeye alisema kwamba wamekamilisha asilimia 90 ya usajili wa Mwinyi Zahera na wachezaji wote ni majembe ambao anaamini klabu hiyo itatisha msimu ujao.
Alisema kwamba kabla ya kuanza ligi watafanya ziara kwenye mikoa mbalimbali ili kutambulisha silaha zao kama ilivyokuwa kwenye utaratibu wa Yanga zamani. Katika hafla ya jana ilihudhuriwa na Wabunge na vigogo mbalimbali wa Serikali huku mgeni rasmi akiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
MWIGULU ALETA JEMBE
Mbunge wa Iramba Magharibi, Dk Mwigulu Nchemba alisema kwenye hafla ya jana kwamba tayari ameshakamilisha usajili wa jembe jipya la ndani ya nchi ambalo litaungana na viungo wengine wa timu hiyo Papy Tshishimbi na Feisal Salum ‘Fei Toto’ kwa ajili ya kupiga kazi msimu ujao.
“Kama nilivyokuwa nimeahidi kuwa nitasajili jembe jingine kwa ajili ya Yanga, tayari nimeshafanya hivyo na jembe hilo ni zaidi ya Fei Toto. Muda ukifika tutalitambulisha,”alisema Mwigulu na Spoti Xtra linajua mchezaji anayemleta ni Kenny Ally wa Singida United
The post YANGA YAISIMAMISHA NCHI appeared first on Global Publishers.
0 Comments