Meneja wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' amesema haikuwa rahisi timu hiyo kumaliza nafasi ya pili ikiwa kwenye mapito ya ukata, jambo alilowapongeza wachezaji kwa ushujaa na uzalendo waliouonyesha msimu huu.
Cannavaro alisema wachezaji wa Yanga walifanya kazi kubwa bila kujali changamoto za kukosa mahitaji yao muhimu na kwamba walidhihirisha utofauti wa uwezo na morali ya kupewa motisha ya kuamsha ari ya mchezo.
Alisema walichokifanya mastaa hao kimeacha alama ya kukumbukwa, akisisitiza kwamba sio jambo jepesi kujitolea bila kujua watapata lini haki zao wakati soka ndilo wanalolitegemea liwapatie uchumi.
"Shujaa ni yule yupo tayari kufanya jambo lenye manufaa kwa wengine hata kama yeye hawezi kupata kitu chochote, ndicho walichokifanya wachezaji wa Yanga waliweka maslahi pembeni.
"Soka ni kazi yao kama ilivyo nyingine, lakini kuna wakati walikuwa wanapitia changamoto lakini hazikuwafanya wakate tamaa, walijituma pengine zaidi ya wale ambao walikuwa na kila kitu ndio maana nasema wanastahili pongezi,"alisema.
Alipoulizwa kwa uzoefu wake ni maeneo gani yanastahili kuongezwa nguvu kwenye kikosi cha Yanga? Alijibu :
"Msimu ujao lazima uwe unalenga ubingwa hivyo lazima wapatikane baadhi ya mastaa wa kuongeza nguvu"
"Siwezi kusema nani asajiliwe ama nani aachwe hiyo ni kazi ya kocha Mwinyi Zahera ndiye anayejua kikosi chake kiwaje kwani anajua ni changamoto zipi alikutana nazo msimu mzima, nadhani analifanyia kazi" alisema.
Cannavaro alisema kikubwa ndoto za msimu ujao ziwe ni ubingwa akidai anaamini viongozi waliopo watakuwa mwanga juu ya kutimiza hilo
"Uzuri ni kwamba ligi inayokuja Yanga itakuwa na utulivu kwa maana ya viongozi wapya ni wa mpira"
"Changamoto kubwa ya msimu uliopita ilikuwa ni ukata pamoja na kuwa na uchaguzi ambao ulikuwa na changamoto za hapa na pale, lakini kwa sasa tunashukuru Mungu kwamba kila kitu kitakwenda sawa kwa maana watu wakumpa sapoti kocha wapo" alisema.
0 Comments