Windows

Ukweli ndivyo ulivyo! Hii kasi ya Yanga SC inavutia, inashtua!

Mwanaspoti, Ukweli, ndivyo ulivyo, Hii kasi, Yanga SC, inavutia, inashtua, Michezo
Kasi hii ya usajili Yanga inashangaza, halafu inavutia. Wababe hao wamerudi kwa kishindo. Imeitetemesha Simba na utajiri wao wote. Fikiria tu, Yanga iliyokuwa ikitaniwa ombaomba ghafla tu, imeibuka kitajiri.

Inafanya usajili wa nyota wapya kwa fujo. Inazitetemesha timu pinzani kwa kasi hiyo ya usajili. Ukilala leo utasikia imemnasa huyu, ukiamka kesho utasikia imeshusha kifaa hiki.

Yaani imerejea katika zile vurugu zao. Vurugu zilizokuwa enzi za kina Francis Kifukwe na ufalme wa Yusuf Manji pale Jangwani. Inashangaza kidogo!

Majuzi tu, ilikuwa ikikabwa koo na nyota wake juu ya malimbikizo ya mishahara na posho, halafu ghafla tu inasajili kila anayekatiza mbele yao. Mpaka jana Jumamosi, tayari sura zaidi ya sita zilishatua Jangwani.

Farouk Shikalo kutoka Kenya ameshasaini. Watson Kalengo wa Zambia naye ndani. Issa Bigirimana, Patrick Sibomana kutoka Rwanda na Burundi nao ndani. Kuna Mghana Lamine Moro na Abdul Aziz Makame na sijui Ally Sonso, watoto wa hapa hapa nyumbani.

Kwa nini isitetemeshe? Kwa nini isishangaze?! Sawa, ni kweli Yanga imepata uongozi mpya na makini chini ya Dk Mshindo Msolla na Fredrick Mwakalebela. Ni kweli Yanga ina vigogo wazito wenye fedha zao. Vigogo wanaoweza kuamua kujitolea kwa hali na mali na kuipaisha timu yao.

Lakini mbona imekuja ghafla namna hii? Kipindi kile kukiwa na migomo baridi walikuwa wapi? Au waliuchuna ili kutaka kuja kivingine kufuta ule ufalme uliotetemekewa Jangwani?

Yaani hata kabla ya ile harambee ya Juni 15 kufanyika, Yanga imezifanya hadi Simba na Azam ziigwaye. Unabisha nini? Juzi kati si mmemsikia Bilionea wa Simba, Mohamed ‘Mo’ Dewji, akisema klabu yao wala haijaanza kufanya usajili?

Nyie mnaamini ni kweli? Mnajua kama Patrick Gakumba aliletwa nchini na kufichwa kule Landmark Hoteli? Unafikiria ni Yanga ndio waliomtumia tiketi kutoka kwao? Hapana! Unadhani ni matajiri wa Azam waliomwalika nchini? Wala! Ni Simba waliomvutia waya na kumwita hasa baada ya kunogewa na mzigo aliowaletea msimu huu.

Meddie Kagere ‘MK14’! Straika aliyechangia sehemu kubwa ya mafanikio ya Simba msimu huu. Amefunga mabao sita yaliyoifikisha Simba robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2018-2019. Amefunga manne yaliyoiwezesha kufika Fainali ya Kombe la Kagame japo walilala mbele ya Azam FC.

Mabao yake 23 yamesaidia kuifanya Simba itetee taji la Ligi Kuu, huku bao lake lilisaidia pia kuipa Simba Ngao ya Hisani pale jijini Mwanza.

Katika msimu wake wa kwanza tu ameifungia jumla ya mabao 39 kwa mechi zote. Kwa nini mabosi wa Msimbazi wasimuite tena Gakumba awaletee majembe mengine kama MK14?
Simba imeingia hofu? Haijui watani wao wamejipanga vipi? Kwani kasi yao ya kutaka kuwang’oa baadhi ya nyota wa Msimbazi waliomaliza mikataba inawatisha.

Imewapa ugumu mkubwa hata kuwasainisha mikataba mipya vijana wao waliomaliza ile ya kwanza. Vijana wao hawataki tena kusaini, wakijua mtaa wa pili kuna neema na pengine napo wataitwa? Hata Azam tumbo linawacheza, hawajui mabosi wa Jangwani wanafikiria nini kuhusu nyota wao ama wale inayowataka kuwasajili. Yanga inawapa tumbo joto.
Kasi ya Yanga upande mmoja imewapa ugumu wapinzani, upande wa pili ni kama inapunguza thamani ya wachezaji kuelekea kwenye usajili.

Ndio, kama Jangwani wanafanya usajili kwa fujo hata kabla ya dirisha halijafunguliwa, pale litakapofunguliwa, kutakuwa na soko gani la wachezaji tena? Yanga itakuwa imeshamaliza kazi.
Simba na klabu nyingine hazitakuwa na hofu tena, zinaweza kuwabana wachezaji inaowataka kwa dau la kawaida kabisa. 

Ukweli ulivyo Simba na Yanga na pengine sasa Azam ndizo zinazopandisha thamani za nyota wa soka nchini. Ndio maana baadhi yao hawafikiria kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi. Sasa kama Yanga imeshafunga usajili, watakimbilia wapi kama sio Simba ama Azam hata kwa usajili wa mali kauli?!
We fikiria tu, Yanga iliyokuwa ikitembeza bakuli, leo inasajili nyota wapya wenye viwango vyao moja kwa moja bila majaribio wala nini, kwa nini isizitetemeshe timu pinzani?

Inawezekana ni zile aibu za kumaliza misimu miwili mfululizo bila taji. Inawezekana zile tambo za Haji Manara zimewakifu, pia huenda ni mpango mkakati ikipania kuonyesha kumbe bila hata Manji ama kutegemea mfuko wa mtu mmoja, Yanga inaweza.
Ni jambo zuri, lakini hofu yangu isije usajili huo wa Jangwani ukawa unafanyika kwa sifa, kisha mbele ya safari ikaibuka ile aibu ya migomo ya nyota wake kwa kukosa mishahara na posho. Isije ikaibuka tena migomo baridi ya kushinikiza kulipwa fedha za usajili.

Kama kweli Yanga imeamua kujivua gamba na kuonyesha kweli wao ni Baba Lao na klabu hiyo ni kubwa kuliko mtu yeyote, basi irekebishe yote yaliyojitokeza ndani klabu hiyo katika misimu miwili ya aibu.

Sambamba na hilo, itengeneze mfumo ambao utaifanya klabu hiyo ije kujiendesha yenyewe bila kuhitaji nguvu ya mifuko ya viongozi na kikundi cha wachache. Itengeneze mfumo ambao itaweza kujiendesha hata kama Dk Msolla na wenzake watakapoondoka kwa kumaliza muhula wa uongozi wao. Mfumo wa kisasa ambao utaifanya Yanga ijiendeshe kwa nguvu zake, kwa vile ina jina kubwa na rasilimali watu wanaoweza kuitajirisha na kuifanya iwe mbali kiuchumi na kimaendeleo tofauti na ilivyo sasa. Ngoja tuone!

Post a Comment

0 Comments