Windows

Twariq Mbongo anayesaka kutoboa England akili yote Taifa Stars

Mwanaspoti, michezo, Twariq Mbongo anayesaka, Tanzania kutoboa England, Mwanasport, Michezo blog
UNAWEZA usiamini lakini unaambiwa kusini mwa jiji la London nchini England kwenye viunga vya Stratford wanakotoka Wagonga Nyundo wa jiji hilo, West Ham United kuwa Wabongo kibao wanaotafuta maisha ya soka.

Twariq Yusuf amefichua hilo kwa kusema amekuwa akikutana na wachezaji wenzake wa Kitanzania wakiwa kwenye akademi mbalimbali za soka nchini humo.

Mwamko kwa Watanzania umekuwa mkubwa katika utafutaji wa maisha ya mpira kwa upande wa wazazi nao kuwasapoti watoto wao kitu ambacho kwa miaka kadhaa nyuma kilikosekana.

Twariq hayupo kusini wala jijini London, yeye yupo Oxford kwenye akademi ya GPS Oxford ila aliona ni vema kuongea nasi hilo kwenye mazungumzo yetu.

“Najiona mwenye furaha na bahati kupata nafasi ya kuwa kwenye kituo cha GPS Oxford, nimekuwa nikifuata mafunzo kwa bidii na kuzingatia masomo kitu ambacho nimekuwa pia nikisisitizwa nyumbani.
“Napenda kuwa mchezaji mkubwa muda wangu ukifika, sitamani kuishia kwenye ngazi ya akademi, ninachojua muda ukifika wa kumaliza wapo ambao wanapata nafasi ya kwenda moja kwa moja kwenye timu lakini wengine huachwa.
“Sina mawazo kwamba nitaachwa hapana, nimesema uhalisia ulivyo, nimekuwa nikijituma ili kuwa bora, nikiwa bora siyo rahisi kukosa timu ya kuichezea,” anasema.
Twariq anasema kuwa amekuwa akikutana na Watanzania wenzake kwenye ligi mbalimbali za vijana kitu ambacho kimekuwa kikimpa faraja ya kucheza na kufarahi nao.
“Sisi ni ndugu kwa hiyo kitu muhimu ni kupendana, ninafahamiana pia na Haji Mnoga ambaye nasikia amekuja Tanzania kwa mapumziko mafupi kabla ya kurejea England kuanza maandalizi ya msimu ujao.
“Ni kaka kwangu na tumekuwa tukiongea, msimu uliopita aliweka rekodi, Portsmouth F.C. nina vitu vingi vya kujifunza kutoka kwake,” anasema kinda huyo.
Haji msimu uliopita aliweka rekodi ya kuwa kinda wa pili kihistoria kucheza mchezo wa ushindani dhidi ya Crawley Town akiwa na Portsmouth F.C ambapo alikuwa na miaka 16, miezi mitano na siku 24.
Ndoto ya Twariq ambaye ni mshambuliaji, ni kucheza Ligi Kuu England ili kuwa msaada kwa taifa la Tanzania kwenye mashindano mbalimbali.
Twariq anasema dua zake kwa sasa ni kutaka Taifa Stars ifanye vizuri kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini Misri ambako tunashiriki kwa mara pili, baada ya miaka 39.
“Nitafuatilia Afcon kwaajili ya Taifa Stars, nitafurahi angalau tukivuka makundi najua yatakuwa mafanikio makubwa kwetu, hilo litatupa ujasiri wa kutembea vifua mbele.
“Haiwezi kuwa rahisi lakini naona tuna wachezaji waofanya vizuri. Nimekuwa nikifuatilia vile ambavyo Samatta amekuwa akifanya vizuri. Kiwango chake kitaisaidia pia timu kushambulia kwa nguvu,” anasema.
Akiyazungumzia maisha ya England na uzito uliopo kwenye soka la vijana, Twariq anasema mafunzo ya kwenye kituo cha soka yaliyopo yana uzito na wamekuwa wakianzia darasani kwa kusoma kabla ya kwenda kuyafanyia kazi kwa vitendo uwanjani.
“Kuna vitu vingi tumekuwa tukifundishwa. Nakumbuka zamani tulikuwa tukifundishwa namna ya kuuficha mpira mguuni, unawezaje kukimbia na mpira, namna ya kugeuka nao.
“Yapo mambo mengi, vingine huwa ni vitu vya zaida ambayo kila mwenye kipaji huzaliwa navyo,” anasema.
Miongoni mwa timu ambazo anatamani kuzichezea Twariq ni Manchester United, Liverpool, Chelsea na Arsenal pindi akianza kucheza soka la ushindani.
“Siwezi kujipangia kwa sababu Mungu naye huwa na mapenzi yake, lakini hizo ni timu ambazo napenda kuzichezea, ikitokea nimepata timu nyingine siwezi kuwa na shaka au kinyongo cha kuichezea,” anasema.
Nyota anaowakubali Ligi Kuu England, Twariq anasema kuwa ni Sergio Aguero wa Manchester City, Mohammed Salah na Sadio Mane wa Liverpool, Harry Kane wa Tottenham Hotspur na Pierre-Emerick Aubameyang wa Arsenal.


Post a Comment

0 Comments