HII sasa sifa, kama ulidhani Yanga wanatania basi itakuwa ulikosea sana, bado mabingwa hao mara 27 wa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara wameendelea kujiimarisha kwa kumwongezea mkataba beki wao wa kushoto, Gadiel Michael.
Tetesi nyingi ambazo zilizagaa hivi karibuni zilidai beki huyo wa Taifa Stars alikuwa akinyemelewa kwa ukaribu na wapinzani wao ambao wanatajwa kuhitaji kusajili beki mwingine wa kushoto.
Hata hivyo, DIMBA Jumatano lilipata habari za uhakika kuwa Gadiel ameongeza mkataba wa miaka miwili wa kuendelea kukipiga Jangwani na sasa yupo katika maandalizi ya michuano ya AFCON itakayofanyika nchini Misri baadaye mwezi huu.
Pia imefahamika beki huyo aliongezewa mkataba hapo jana baada ya shinikizo kubwa la kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, ambaye yupo kwenye maandalizi ya timu ya Taifa ya DR Congo hivi sasa kuelekea Misri.
“Gadiel Michael jana ameongezewa mkataba wa miaka miwili ikiwa ni moja ya wachezaji ambao Zahera alipendekeza waendelee kuwepo,” alisema kocha huyo alipoulizwa na gazeti hili.
Mpaka sasa Yanga imefanya usajili wa wachezaji zaidi ya watano huku Papy Tshishimbi akiwa mmoja wa nyota walioongezewa mkataba wa kuendelea kuicheza timu hiyo.
0 Comments