Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuanzia Julai Mosi mwaka huu Serikali itaanza kutekeleza Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara nchini (Blueprint) kwa lengo la kurahisisha mazingira ya kufanya biashara.

Waziri Mkuu ameyasema hayo Ijumaa hii, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, jijini Dodoma. Amesema wakati kazi hiyo inaendelea Serikali itafanya ufutialiaji kuhusu utekelezaji wa mpango huo na kutathmini kama lengo limefikiwa.

”Utekelezaji wa mpango huo unakwenda sambamba na dhamira ya Serikali ya kurahisisha mazingira ya kufanya biashara nchini, unaojidhihirisha kupitia sheria ya fedha ya mwaka 2019 ambayo imefuta tozo kwamishi 54 zilizobainishwa kwenye mpango huo.”

Waziri Mkuu ametaja tozo zilizoondolewa au kupunguzwa ni pamoja na zinazosimamiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Wizara ya Mifugo na Uvuvi hususan kwenye Sekta ya Mifugo, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Maji.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema katika kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo unaleta tija, ameielekeza Wizara ya Viwanda na Biashara ishirikiane na Ofisi ya Waziri Mkuu kusambaza blueprint pamoja na Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa wizara zote kwa ajili ya kusimamia utekelezaji katika maeneo yao.

Amesema kupitia mpango wa bajeti ya 2019/2020, Serikali itaendelea kuweka mazingira rahisi ya ufanyaji biashara kwa kutoa unafuu katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi pamoja na shughuli nyingine jumuishi.