Mwenyekiti wa Kamati ya uongozi ya Ofisi ya Mpango wa kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA ) Balozi mstaafu, Daniel Ole Njolay amewataka Wananchi waliokabidhiwa Hati za Ardhi kuzitumia vyema kwa ajili ya kuombea Mikopo itakayowasaidia kupambana na umasikini wa kipato.
Balozi Njolay ametoa wito huo katika hafla ya kuwakabidhi Wananchi 54 wa Mpendae mjini Zanzibar Hati hizo mara baada ya kukamilisha masharti ya usajili.
Amesema Serikali ya Muungano kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeazimia kuwakomboa Wananchi wake na umasikini wa kipato kupitia njia mbali mbali ikiwemo kuwapatia Hati za Ardhi zitakazowasaidia katika harakati zao za kimaendeleo.
Amewataka Wananchi hao kuzitumia Hati hizo ili kuomba Mikopo kutoka vyanzo mbalimbali vya kifedha ikiwemo Benki kwa ajili ya kuendeshea maisha yao.
“Wenzetu nje ya nchi Hati hizi zinakuwepo katika Bank huzitumia kikamilifu kukomba Mikopo ya kuwasaidia kuendeleza miradi yao ya kimaendeleo ambayo wanaianzisha hivyo hapa Tanzania tunawajibu wa kuyaiga hayo, ” amefahamisha Balozi Njolay.
Kwa upande wake Mratibu wa MKURABITA Tanzania Dkt. Seraphia Mgembe amewaomba Wananchi hao hasa Wazee kuzitumia Hati hizo ili kukamilisha ndoto zao walizoshindwa kuzifanya wakati wa ujana wao.
0 Comments