Nahodha wa timu maarufu ya soka Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Sinza Boys Veterani, Ali Ngoti amesema licha ya kufungwa 4-3 na Timu ya Global FC, wanaamini mechi inayofuata watalipa kisasi kwani hawadhani wao ni wa kufungwa kirahisi.
Akizungumza na mtandao huu, Ngoti alisema timu yao ilikuwa imejipanga kwa ushindi mnono lakini makosa madogo waliyofanya ndiyo yaliyosababisha washindwe kung’ara.
“Global FC ni timu nzuri sana, wachezaji wake wanajua kutandaza soka lakini sisi licha ya ukongwe wetu, hatuamini kwamba ni wa kufungwa kirahisirahisi.
“Tunakwenda mafichoni, tukiibuka tunataka mechi tena na naamini tutalipa kisasi, sisi siyo wa mchezomchezo, waliowahi kucheza na sisi wanajua mziki wetu, kwa hiyo Global wajipange kweli, safari nyingine tukikutana tunawaaibisha,” alisema Ngoti.
Naye kepteni wa Global FC, Wilbert Moland alisema: “Kipigo cha bao 4-3 walichokipata Sinza Veterani kiliwastahili, kama wanaona tulibahatisha, wajipange upya, nakuhakikishia tukikutana tena tunawapiga hamsa.”
Sinza Boys Veretani na Global FC inayodhaminiwa na Kampuni ya Ashishi Cinematographer walikipiga kwenye uwanja wa Mashujaa uliopo Sinza Kumekucha na wanatarajiwa kurudiana hivi karibuni.
Aidha, Global FC ambayo mwaka huu imefanya usajili wa kutisha iko kambini ikijiandaa na mechi na timu kubwa Bongo. Ni timu gani hiyo? Kaa mkao wa kusikilizia. Kumbuka michezo ni afya!
Imeandikwa na Amran Kaima.SAID ALLY, Dar es Salaam
The post Global FC Yailambisha Mchanga Sinza Veterani appeared first on Global Publishers.
0 Comments