Windows

Beki mpya Yanga awatumia salamu washambuliaji Ligi Kuu



Beki mpya wa Yanga, Seleman Mustapha, amewatahadharisha mastraika wa Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa wasitarajie kupata nafasi ya kufunga kirahisi pale atakapoanza kucheza katika klabu hiyo.

Mustapha ambaye ni raia wa Burundi, amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Yanga msimu ujao, akitokea klabu ya Aigle Noir ya nchini kwao.

Mustapha alisema, Ligi ya Tanzania ina ushindani mkubwa hivyo atakuwa makini ili aweze kupambana nayo.

"Nakuja Tanzania kupambana, hivyo nitahakikisha ninaisaidia timu yangu iweze kupata matokeo mazuri na kufikia malengo," Mustapha aliliambia gazeti la Bingwa

"Ninafahamu kuna washambuliaji hatari, akiwemo Meddie Kagere, John Bocco na wengineo, lakini hilo halinisumbui kwani nitakuja kupambana, mashabiki wa Yanga wasiwe na wasiwasi"

Alisema amekuwa akiifuatilia kwa ukaribu ligi ya Tanzania hivyo kuna wachezaji wengine ambao anawafahamu kama Ibrahim Ajib, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ wa Yanga na wengineo.

Beki huyo wa timu ya Taifa ya Burundi, anayemudu kucheza namba tano na namba sita, alisema anafurahi kuja kucheza Yanga, hivyo mashabiki wa timu hiyo, wategemee mambo mazuri zaidi.

Yanga imeshawasainisha baadhi ya wachezaji, wakiwemo, beki Lamile Moro kutoka Ghana, mawinga Patrick Sibomana na Issa Bigirimana wote kutoka Rwanda, Ally Mtoni ‘Sonso’ (Lipuli FC) na Abdulazizi Makame (Mafunzo, Zanzibar).

Kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, mchakato wa usajili bado unaendelea, akitamba kushusha vifaa vya nguvu ambao wote wanachezea timu zao za Taifa

Post a Comment

0 Comments