REWIND! Ni miaka sita tangu alipofariki dunia mfalme wa freestyle kwenye muziki wa Hip Hop Bongo, Albert Kenneth Mangweha ‘Ngwea’, lakini bado familia yake inalalama juu ya kifo cha mpendwa wao, Risasi Mchanganyiko lina habari ya kipekee (exclusive). Mei 28, ndiyo huwa ni kumbukizi ya kifo hicho kilichoacha utata mkubwa kwa namna kilivyotokea na pengo lisilozibika kwenye muziki wa Bongo Fleva kilichotokea ghafla Mei 28, 2013 huko Johannesburg nchini Afrika Kusini.
RISASI LATINGA
Katika kumbukizi ya kifo cha Ngwea wiki iliyopita, Risasi Mchanganyiko lilitinga nyumbani kwa mama mzazi wa Ngwea, Denisia Magweha ambaye alifunguka mapya juu ya kifo cha mwanaye huyo.
Baada ya kushiriki misa kisha kuweka shada la maua kwenye kaburi la Ngwea lililopo Makaburi ya Kihonda mjini Morogoro, gazeti hili lilifika nyumbani kwa mama huyo maeneo ya Mazimbu- Road, Kihonda na kufanya naye mahojiano maalum.
Risasi Mchanganyiko: Mama habari za siku nyingi?
Mama Ngwea: Nzuri tu, ninamshukuru Mungu ninaendelea vizuri.
ANAMMISI NGWEA
Risasi Mchanganyiko: Ni miaka sita tangu alipofariki dunia Ngwea, je, una neno lolote kwa wanamuziki wenzake?
Mama Ngwea: Kwanza niseme tu ukweli kwamba ninammisi sana Albert (Ngwea). Ni kweli ni miaka sita, lakini bado namuona yupo moyoni mwangu siku zote.
Unajua mwanzoni ilikuwa ngumu sana kuamini kwa sababu taarifa za kifo chake zilikuwa za ghafla sana. Nakumbuka ilikuwa ni miaka mitatu kama sikosei nilikuwa nimempoteza baba yake (Keneth Mangweha, kaburi lake lipo mita tatu kutoka kwenye kaburi la Ngwea).
Kwa hiyo ndani ya kipindi kifupi nikawa nimepoteza watu wangu muhimu sana. Nadhani unaweza kuona ni kwa jinsi gani nilivyoumia. Kiukweli nilimpenda, ninampenda na nitaendelea kumpenda siku zote. Kifupi ninammisi sana.
MAPYA KIFO CHA NGWEA
Risasi Mchanganyiko: Mama naomba nikurudishe nyuma kidogo, wakati kifo cha Ngwea kilipotokea kuliibuka taarifa nyingi za utata juu ya kifo chake, je, mpaka leo familia inajua ni nini hasa kilimuua Ngwea?
Mama Ngwea: Ukiachilia mbali cheti cha kifo cha Albert (Ngwea) tulichopewa siku kadhaa baada ya mazishi, hatujawahi kuelezwa kwa kina juu ya kile kilichomsababishia mauti au hata mwenendo wa kesi au uchunguzi wa kifo chake.
Ni kweli, kama familia, mara kadhaa tulikutana kwenye vikao vya ndani na kukubaliana kulifuatilia suala hilo katika Ubalozi wa Afrika Kusini jijini Dar. Huko alikwenda baba mdogo wa Albert (David Mangweha) na kukumbana na vizingiti kibao kwamba ripoti ya kifo chake ilikataliwa kutolewa nchini humo (Afrika Kusini).
Nakumbuka alipokwenda ubalozini hapo kwa mara ya mwisho aliambiwa aandike barua ya kuomba kujua kinachoendelea ikiwa ni pamoja na ishu ya kama kuna kesi yoyote kwenye kifo chake ili kama alidhulumiwa uhai ambao ni haki yake, basi haki itendeke.
Lakini hakuna kilichoendelea hivyo ukiniuliza hapa ni nini kilimuua mwanangu siwezi kukuambia maana tulipewa cheti cha kifo tu bila maelezo ya chanzo cha kifo chake.
Wakati mwingine tulidhani huenda ripoti hiyo ilikwama sehemu au uchunguzi ulikuwa haujakamilika, lakini siku zilisonga tukaona kimya hivyo kama familia tumeamua tu kumwachia Mungu kama ilikuwa ni mipango yake, basi itimie.
Risasi Mchanganyiko: Je, ulishanufaika kiasi gani na kazi za Ngwea?
Mama Ngwea: Ni kweli nasikia nyimbo zake zikipigwa na kuona kwenye runinga. Pia nina hati na haki miliki ya nyimbo zote za Albert. Hiyo hati ya kazi zake zote ninayo ndani, lakini sijawahi kupata chochote kwa maana ya pesa hivyo nawaomba watu wanaotumia kazi hizo wawasiliane na mimi.
Pia namuomba Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo (Dk Harrison Mwakyembe) na Rais John Pombe Magufuli ambaye ninaamini ni mtetezi wa wanyonge wanisaidie angalau na mimi nipate chochote. Pia kwa yeyote anayetaka kutumia kazi za mwanangu kwa ajili ya matamasha anaruhusiwa, lakini awasiliane na mimi.
Naomba nieleweke kwamba sikatai kazi za mwanangu kutumika na yeyote anayetaka kuandaa tamasha au chochote kwa kutumia kazi hizo, basi ni rahisi tu awasiliane na mimi hatutashindwana ili na mimi niambulie chochote.
Risasi Mchanganyiko: Ni nyimbo gani za Ngwea ukizisikia huwa unamkumbuka?
Mama Ngwea: Nyingi tu nikizisikia namkumbuka kama She Got A Gwan ni wimbo mzuri kwa sababu unazungumzia upendo wa kweli jinsi mtu akiwa na mpenzi wake wanavyoweza kusameheana au kuchukuliana katika upendo na ndiyo maisha yanavyokuwa kati ya watu wawili wanapokuwa pamoja.
Wimbo huo nilianza kuusikia kwenye redio, alipokuja hapa nyumbani nikamwambia wimbo wako kweli mzuri na umetoka vizuri akacheka kwa sababu yeye alikuwa mtu wa kucheka tu, ukimwambia kitu cha kufurahisha alikuwa anacheka na kusema poa tu mama.
Risasi Mchanganyiko: Unawaambia nini wanamuziki wenzake?
Mama Ngwea: Mimi nawaambia wote pamoja na ninyi Global, msinisahau hadi mje kwenye kumbukizi tu, mnikumbuke mara kwa mara.
NGWEA NI NANI?
Ngwea alizaliwa Novemba 16, 1982 jijini Mbeya, Tanzania. Kiasili Ngwea alikuwa mtu wa Ruvuma yaani Mngoni. Lakini alizaliwa jijini Mbeya na akiwa na umri wa miaka mitano, familia yake ilihamia mjini Morogoro kikazi na hatimaye kuanza masomo ya msingi hadi darasa la tano.
Alipata uhamisho wa kwenda jijini Dodoma ambapo alijiunga na shule ya Msingi ya Mlimwa kisha S
ekondari ya Mazengo na Chuo cha Ufundi cha Mazengo. Katika ngazi ya familia, Ngwea alikuwa mtoto wa mwisho (kwa baba akiwa mtoto wa 10) na (kwa mama akiwa mtoto wa sita). Ngwea alifariki dunia Mei 28, 2013, nchini Afrika Kusini.
SAFARI YA MUZIKI
Ngwea alikuwa akiishi Sinza, Dar baada ya kuhama jijini Dodoma alikokuwa na Kundi la Chamber Squared lililoundwa na yeye mwenyewe, Noorah, Dark Master na Mez B ambaye naye ametangulia mbele ya haki.
Akiwa jijini Dar, Ngwea alikokutana na mtayarishaji mahiri wa muziki wa Bongo Fleva, P Funk Majani na kuanza kufanya naye kazi. Hiyo ilikuwa ni mwaka 2003 ambapo alitoa wimbo wake wa kwanza ulioitwa Ghetto Langu uliompatia umaarufu mkubwa. Kupitia muziki wake, Ngwea aliwahi kutwaa Tuzo ya Kilimanjaro kama mwana- HipHop na Albam Bora ya Mimi. R.I.P Ngwea!
The post BAADA YA MIAKA 6 MAMA AIBUA MAPYA KIFO CHA NGWEA appeared first on Global Publishers.
0 Comments