Windows

Yanga yaahirisha Harambee ya May 18

Uongozi wa Yanga umeahirisha tukio kubwa la Harambee lililokuwa limepangwa kufanyika Hotel ya Serena Jumamosi, May 18 kutokana na waumini wa dini ya Kiislam kuwa katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani


Akizungumza na waandishi wa Habari mapema leo, Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla amesema, tukio hilo litafanyika baada ya sikukuu ya Idi kupita
"Watanzania wengi wako kwenye mfungo wa mwezi wa Ramadhani kwa hiyo tumeona umoja ni nguvu, ukianza kufanya shughuli ya Harambee kubwa hatutafanikiwa kama baadhi ya Watanzania wenzetu wako kwenye mfungo," amesema
"Kwa hiyo tumeahirisha, tusogeze muda, baada ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani tutatafuta tarehe ili tuweze kuwa na Harambee kubwa"
"Lengo letu ni lilelile, klabu kuwa na pesa ya kutosha ya usajili ambayo benchi la ufundi watakabidhiwa kwa ajili ya kujenga kikosi imara na cha ushindani kwa ajili ya msimu ujao"
Dk Msolla amewataka Wanayanga waendelee kuichangia timu yao, wapuuze taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa timu hiyo imepata mfadhili
"Wanachama wa Yanga msikatishwe tamaa au kupewa imani kuwa tumepata mwekezaji mkaacha kuichangia timu yenu"
"Hatuna mkataba wala mazungumzo na mtu yeyote. Najua wenye dhamira iyo wapo lakini taratibu hizo bado hazijafikiwa. Kwa hiyo tuendelee kuchangia, hakuna pesa ambayo tumeahidiwa wala kuanza mazungumzo na mtu yeyote"
Katika hatua nyingine, Dk Msolla ametangaza kuongezwa kwa wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji ambao wanafanya idadi ya Wajumbe hao kufika kumi
"Wajumbe wawili tumewaongeza leo kupitia nafasi za uteuzi wa Mwenyekiti ambao ni Dk Athumani Kihamila ambaye ni Mkurugenzi wa Tume ya uchaguzi na Shija Richard ambaye ni Meneja wa TRA. Tunaendelea na mchakato wa kuongeza wajumbe wengine lakini kwa sasa tumeanza na hao wawili"

Post a Comment

0 Comments