Windows

Yanga ilikwama hapa tu

SIMBA ndio mabingwa wapya 2018-19 wakitetea  kwa mafanikio taji lao walilotwaa msimu uliopita.
Kwa mara ya pili mfululizo, Simba wanalibeba taji hilo wakiwa mkoani Singida, wakiwa wamebakisha mechi mbili ili  kumaliza msimu huu.
Ni taji la 20 la Ligi Kuu ya Bara kwa Wekundu wa Msimbazi wakizidi kupunguza pengo lililokuwapo dhidi ya mabingwa wa kihistoria wa taji hilo, Yanga waliolibeba mara 27.
Mbio za nyika, mabonde na milima katika kuwania taji hilo zimefikia tamati baada ya Wekundu wa Msimbazi kuthibitisha kwamba wao ndio wafalme wa soka la Bongo kwa msimu wa pili mfululizo.
Ufalme wa Simba msimu huu umepatikana baada ya miamba hao kupoteza mechi tatu tu za ligi, mbili dhidi ya Kagera Sugar na moja dhidi ya Mbao FC ya Mwanza. 
Simba imefikisha alama 91 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote ikiwamo waliokuwa wapinzani wao katika mbio za ubingwa, Yanga ambao kabla ya mechi ya jana, walikuwa na alama 83 baada ya michezo 36 kila mmoja.
Hata hivyo, watani wamebakisha michezo miwili kila mmoja huku ubora wa Simba ukichagizwa na upana wa kikosi chao tofauti na watani zao Yanga.
Mambo hayako sawa ndani ya klabu ya Yanga yenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam.
Yanga imeyumba ule ufalme wa miaka mitano sasa haupo tena, hawana chochote walichoambulia msimu huu.
Si taji la Ligi Kuu Tanzania Bara pekee walilolikosa hata nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho mwakani wameikosa, baada ya kutolewa katika Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC).
Zipo sababu nyingi zilizochangia Yanga kuambulia patupu msimu huu, BINGWA leo linaainisha chache ambazo zimesababisha vijana hao wa Wanajangwani kutoka kapa.
Ukata
Yanga waliishi miaka 11 kitajiri. Walikuwa wanakula pesa za Yusuph Manji kama zao tu. Walisajili mastaa kibao kutoka nje n.k. Walilitawala soka hasa, hakuna mchezaji aliyelia njaa.
Lakini, Yanga ya misimu miwili imepita kipindi kigumu sana tangu mwenyekiti wao apate misukosuko na mpaka sasa kuna baadhi ya mambo hayajakaa sawa.
Kukauka kwa pesa ndani ya timu hiyo ni sababu inayopelekea kuchelewa kulipa mishahara kwa wakati, kitendo ambacho kiliondoa morali ya kujituma.
Kukosa pesa ni kuwanyima uhuru wa kuchagua kambi za kuwaweka wachezaji wao kwa maandalizi ya mechi mbalimbali zinazokuwa mbele yao.
Majeraha
Asilimia kubwa ya nyota ambao walikuwa nguzo kwenye kikosi cha kwanza, walisumbuliwa na majeraha mbalimbali.
Mastaa hao ni Amisi Tambwe, Thaban Kamusoko, Ibrahim Ajib,  Gadiel Michael, Juma Abdul na Juma Mahadhi ambaye hajacheza mechi hata mechi moja msimu huu.
Lipuli ilifuta matumaini yao
Yanga iliondolewa na Lipuli FC kwenye Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC), tumaini pekee walilokuwa nalo wanajangwani hao.
Kipigo cha mabao 2-0 walichopata kwa Lipuli, kilitosha kufuta matumaini yao ya kutwaa Kombe la Shirikisho, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa.
Sasa Lipuli FC itamenyana na Azam FC katika mchezo wa fainali ya michuano hiyo itakayofanyika kwenye Uwanja wa Ilulu mjini Lindi mapema mwezi ujao.   
Usajili 
Inawezekana wengi hawakuliona hili kwa jicho la tatu, lakini ukweli ni kwamba Yanga ile iliyokuwa fiti ilikuwa na kikosi imara mno na ndiyo maana iliweza kutwaa ubingwa kwa miaka mitatu mfululizo na kushiriki vizuri kwenye michuano ya kimataifa hadi hatua ya makundi Kombe la Shirikisho.
Hebu angalia kikosi hiki kuanzia golini walikuwapo Deogratias Munishi ‘Dida’ au Ali Mustafa Barthez, wote hawa ilikuwa wakipangwa bila wasiwasi. Kwa upande wa mabeki, Juma Abdul kulia ama Haji Mwinyi Mngwali kushoto. Katikati alikuwapo Kelvin Yondani na Vincent Bossou, huku kiungo namba sita akiwa ni Thaban Kamusoko, yule aliyekuwa bora kabla ya kuumia na ambaye alisaidiana na Haruna Niyonzima.
Mawinga walikuwa ni Simon Msuva na Deus Kaseke au Obrey Chirwa, huku washambuliaji wakiwa ni Amis Tambwe pamoja na Donald Ngoma.
Lakini baada ya msimu kumalizika, Dida, Barthez, Bossou, Niyonzima, Msuva na Kaseke wote waliondoka pamoja na kocha wao Mholanzi, Hans van der Pluijm. Ndipo Yanga ikaanza kufanya usajili wa kuungaunga. Uongozi ukaanza kukuna kichwa kuona jinsi ya kujaza nafasi zao.
Na hii ni baada pia ya kikosi kilichobaki kuwa na wachezaji majeruhi wengi ambao nafasi zao zilipaswa kuzibwa pia.
Hapa ndipo waliposajiliwa akina Klaus kindoki, Mohammed Issa ‘Banka’, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Deus Kaseke, Mrisho Ngassa, Haruna Moshi ‘Boban’ na  Heriter Makambo.
Usajili ambao wengi wanadai haukukidhi viwango kwa asilimia 100. 

Post a Comment

0 Comments