Windows

YANGA HATARI



YANGA wamebuni mbinu mpya itakayowawezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kuwakata maini watani wao wa jadi, Simba, wanaopewa nafasi kubwa ya kufanya hivyo.

Katika mbio za ubingwa wa ligi hiyo, Simba ipo kileleni mwa ligi hiyo ikiwa na pointi 85 baada ya kucheza mechi 34, huku Yanga ikishika nafasi ya pili na pointi zake 83 ilizovuna ndani ya michezo 36.

Kutokana na hali hiyo, Simba ndio wanaoonekana kuwa na nafasi kubwa ya kubeba ‘mwali’ wa ligi hiyo, huku Yanga wakisubiri miujiza kuona kama wanaweza kupindua matokeo.

Lakini wakati watu wa Yanga wakionekana kukata tamaa ya ubingwa, wamepewa mbinu ‘bab kubwa’ inayoweza kuwashangaza wengi na mwisho wa siku kombe kutua Jangwani.

Mbinu hiyo si nyingine, bali ni kupiga dua kabambe ili timu yao iweze kushinda mechi zake, huku wakiiombea Simba ifanye vibaya.

Aliyetoa mbinu hiyo si mwingine, bali ni nahodha wa zamani wa Yanga ambaye kwa sasa ni Meneja wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Akizungumza na BINGWA jana, Cannavaro, alisema kwa sasa kilichobaki kila mchezaji, shabiki na mwanachama wa Yanga anachotakiwa ni kupiga dua ya nguvu ili wao washinde mechi zao zote na kuwaombea Simba wapoteze.

“Kimsingi kila mtu hapa kwa imani yake, anatakiwa kuomba Simba ifungwe na ninaamini hilo linawezekana kwa wale ambao wana imani. Mwisho wa siku na sisi tushinde tuwe mabingwa, ngoma bado mbichi,” alisema Cannavaro.

Kikosi cha Yanga leo kitaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini, Dar es Salaam, ikiwa ni baada ya mapumziko ya siku mbili waliyopewa na Kocha Mkuu wao, Mwinyi Zahera.

Wachezaji wa Yanga leo wanatarajia kuendelea na mazoezi hayo kujiandaa na michezo yao miwili ya ligi iliyobaki, wakiwa chini ya kocha msaidizi, Noel Mwandila, kwani Zahera yupo nje ya nchi.

Akizungumza na BINGWA jana, Mwandila, alisema yupo tayari kwa ajili ya kuwapa vitu adimu alivyoachiwa na bosi wake, Zahera.

“Baada ya mapumziko ya siku mbili leo tunaendelea na mazoezi kwa ajili ya kumalizia michezo yetu miwili iliyobaki kwa kishindo,” alisema Mwandila.

Kwa upande wake, mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh, alisema michezo yao miwili iliyobaki dhidi ya Azam FC na Mbeya City ndiyo itakayoamua hatima ya ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Tumejipanga kushinda michezo yote na leo wachezaji wote wameambiwa waje kwa wingi mazoezini, hakuna kutega kwa sababu tunataka kumaliza ligi kwa kishindo ndipo mengine yafuate,” alisema Hafidh.

Post a Comment

0 Comments