


KIUNGO wa Ajax, Frenkie de Jong, ameagwa kifalme na mashabiki wa timu hiyo wakati akijiandaa kwenda kujiunga na klabu yake mpya ya Barcelona.
Kiungo huyo Mholanzi alikuwa na mchango mkubwa hadi Ajax ilipofanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo, Eredivisie, na aliiwezesha kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wakati ada yake ya usajili ya pauni milioni 65 ikitarajiwa kuisaidia Ajax kutafuta mbadala wake, maelfu ya mashabiki walijitokeza juzi kumuaga huku wakiimba jina lake.
Kwa sasa Ajax inahangaika kuwabakiza nyota wake wenye vipaji kutokana na nguvu yao ndogo ya kushindana na klabu tajiri za Hispania na England.
Kumekuwa na tetesi pia kuwa huenda Ajax ikampoteza na beki wao wa kati, Matthijs de Ligt ambaye anasakwa na Barcelona ambayo tayari imeshamsajili De Jong.
Jarida la Mundo Deportivo liliripoti hivi karibuni kuwa tayari dili la De Ligt kuhamia Nou Camp kivitendo limeshakamilika na kilichobaki ni klabu zote mbili kukamilisha taratibu.



0 Comments