Windows

YANGA BALAA


YANGA wameendelea kuonyesha jeuri yao ya fedha baada ya jana kushusha vifaa viwili matata ambao walitarajiwa kusaini mkataba muda wowote kabla ya jua kuchomoza leo.

Kati ya wachezaji hao, yupo beki wa kushoto kutoka Rayon Sports ya Rwanda, mwenye uwezo mkubwa wa kupanda kusaidia mashambulizi, akiwa na shabaha ya kufunga mabao hata kuliko baadhi ya straika wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Beki huyo si mwingine, bali ni Eric Rutanga, ambaye tayari ametua nchini ili kumalizana na Wanajangwani hao.

Habari kutoka kwa mmoja wa viongozi wa Yanga, zinasema kuwa Rutanga anadaiwa kuwa chaguo la Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, ambapo iwapo atamalizana na wakali hao wa Jangwani, msimu ujao atakuwa ndani ya jezi za rangi ya njano na kijani.

Mbali ya Rutanga, kifaa kingine kinachotarajiwa kushushwa na Yanga kimya kimya, ni Jonathan Chinze kutoka Nigeria ambaye muda wowote kuanzia sasa, atatua nchini kumalizana na klabu hiyo.

Lakini pia, kipa anayetarajiwa kuwapo katika michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 2019), akiwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Aaron Kalambo, naye anaelezwa kuwa njiani kusaini Jangwani.

Kigogo mmoja wa ngazi ya juu Yanga, ameliambia BINGWA kuwa wanaamini wachezaji hao na wengine waliowasajili watakifanya kikosi chao kuwa tishio msimu ujao.

“Tulishasajili wachezaji wanne wapya na wengine wawili tunamalizana nao leo (jana). Kati yao, yupo beki wa Rayon Sports ya Rwanda, Rutanga Eric, lakini pia kipa wa Tanzania Prisons aliyeitwa Stars, Aaron Kalambo,” alisema kiongozi huyo ambaye aligoma jina lake kuwekwa wazi.

Lakini wakati uongozi mpya wa Yanga chini ya Mwenyekiti, Dk. Mshindo Msolla na kocha wao, Zahera wakiendelea na usajili kwa kasi, mashabiki wa klabu hiyo wamewaonya kutokurupuka katika hilo.

Wakizungumza na BINGWA jana, baadhi ya mashabiki hao, wakiongozwa na Shaaban Omari wa Keko Machungwa, Dar es Salaam, walisema kuwa wana wasiwasi fedha walizonazo huenda zikawafanya viongozi wao kusajili kila mchezaji wanayeletewa bila kujali mahitaji.

“Ndani ya siku chache tayari kuna wachezaji zaidi ya watano wameletwa na tunasikia wamesajiliwa, nadhani viongozi wetu wanatakiwa kuwa makini katika jambo hili.

“Ni vema wakasajili wachezaji wachache kulingana na mahitaji, ukizingatia msimu ujao hatushiriki michuano ya kimataifa. Unaweza kusajili wachezaji kwa pupa, kumbe wengi wao ni vilaza, halafu upoteze fedha kuvunja mikataba, hii ni hatari,” alisema Omari.

Aliwashauri viongozi wao kusajili wachezaji wachache wa kigeni ili kama wakipata wazuri zaidi hapo baadaye, waweze kuwaongeza katika dirisha dogo.

Post a Comment

0 Comments