


VIONGOZI wa Simba ni wajanja sana asikwambie mtu, kwani wakati wenzao wa Yanga wakionekana kuwa na mzuka wa usajili wa wachezaji, hasa wa kigeni, wao wamepozi wakipanga kuibuka kwa kishindo kitakachowaacha midomo wazi mashabiki wao.
Msimu huu Simba ilikuwa na kikosi cha nguvu kilichosheheni wachezaji wazoefu na wenye viwango vya juu, wakiwamo wa ndani na wa kigeni ambao mwisho wa siku, wameiwezesha timu hiyo kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Wakifahamu kuwa msimu ujao watashiriki michuano hiyo ya Afrika, Simba wamepanga kufanya usajili kwa utulivu wa hali ya juu kuhakikisha wanawanasa wachezaji bora zaidi ili kuongeza nguvu kwa wale watakaowabakiza.
Hivyo pamoja na Yanga kuanza kwa kasi mchakato wa usajili, wao wameendelea kupiga hesabu wakipanga kuitikisa nchi kwa kushusha wachezaji wa kiwango cha juu kwa gharama yoyote ile.
Katika kile kilichoonekana ‘kuwa-beep’ wapinzani wao, Simba wanatarajiwa kushusha nchini kiungo mshambuliaji hatari wa klabu ya KCCA aliyeiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchini kwao Uganda.
Mchezaji huyo si mwingine, bali ni Sadam Ibrahim Sadam, ambaye anatarajiwa kutua nchini muda wowote kuanzia sasa.
Akizungumza na BINGWA jana, mmoja wa viongozi wa Simba, alisema wamepanga kuwa watulivu mno katika suala zima la usajili.
“Hatutakurupuka katika usajili, tumepanga kuwa makini sana kwani lengo letu ni kusajili wachezaji wazuri zaidi ya hawa tulionao ili msimu ujao tuweze kufanya vizuri zaidi ya msimu huu katika michuano ya Afrika,” alisema kiongozi huyo.
Alipoulizwa juu ya Sadam, alisema: “Kuna mchezaji nimeambiwa anatoka KCCA ya Uganda, lakini bado sijafahamu jina lake, ila nimeambiwa ni kiungo, akifika tutawajulisha.”
Aliwataka mashabiki wa Simba kutobabaishwa na usajili aliouita wa pupa unaofanywa na watani wao Yanga, akitamba muda ukifika, wanaweza kushusha vifaa vya nguvu hata saba ndani ya saa 24 tu.



0 Comments