


BAADA ya kushindwa katika Uchaguzi Mkuu wa Yanga, aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Yono Kevela, amesema kampuni yake ya Yono Auction Mart ipo tayari kushirikiana na uongozi wa sasa kuwakamata walanguzi wa jezi.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Mei 5 mwaka huu, Kevela alipata kura 30, huku Fredrick Mwakalebela, akiibuka mshindi katika nafasi ya makamu mwenyekiti baada ya kuzoa kura 1,206.
Akizungumza na BINGWA jana, Kevela ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Njombe (Njorefa), alisema yupo tayari kuwasaidia Yanga kuwakamata watu wanaotumia vibaya nembo ya timu hiyo.
“Uwezo wa kufanya hivyo kupitia kampuni yangu hii ya minada ninao kwa sababu kuna watu ambao hawaitakii mema klabu, wamekuwa wakiitumia vibaya nembo ya timu,” alisema Kevela.
Pia Kevela alisema endapo atapewa nafasi hiyo, atahakikisha anawabana vilivyo wauza jezi ambao wamekuwa hawaitendei haki klabu hiyo ya Yanga.
Alisema kuna watu ambao wamekuwa wakijihusisha na kufanya biashara ya jezi za Yanga pasipo klabu hiyo kufaidika na ‘senti’ yoyote.
Kutokana na ufisadi huo, Kevela alisema milango ipo wazi kwa viongozi wa sasa chini ya mwenyekiti, Mshindo Msolla, kumshirikisha juu ya kuwabana wafanyabiashara ambao wamekuwa hawana msaada wowote ndani ya klabu hiyo.
“Nina kazi kubwa ya kupambana na walanguzi wa jezi, hivyo basi endapo mwenyekiti (Msolla) ataona kuna haja ya kuwakamata walanguzi hao nitahakikisha kila kitu kinakwenda sawa,” alisema Kevela.
Kwa muda mrefu Yanga imekuwa ikihaha namna ya kujikomboa kiuchumi licha ya klabu hiyo kuwa na rasilimali nyingi ikiwemo Uwanja wa Kaunda na majengo yake yaliyopo mitaa ya Jangwani na Mafia, Dar es Salaam.



0 Comments