Windows

Wawa: Nitaiwahi mechi ya Sevilla

BEKI wa Simba, Pascal Wawa, amewapa matumaini mashabiki wa Simba atakuwa fiti kuikabili Sevilla ya Hispania ambao wataletwa nchini na Kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa Tanzania.

Aidha, beki huyo raia wa Ivory Coast alisisitiza anaendelea na mazoezi kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam na hivi karibuni anaweza kuanza mazoezi chini ya kocha wao wa viungo, Adel Zrane.

Wawa aliumia katika kipindi cha kwanza mchezo wa robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe na nafasi yake kuchukuliwa na Jjuuko Murshid.

Akizungumza na BINGWA jana, Wawa alisema kuna uwezekano mkubwa hadi kufikia mchezo wao dhidi ya Sevilla, akawa yuko sawa kwani tayari ameshaanza kufanya mazoezi chini ya usimamizi wa madaktari.

Aliwataka mashabiki wake kuondoa hofu juu yake kwa sababu hayuko katika maumivu makali ambayo yanaweza kumfanya kukaa nje muda mrefu.

“Kwa uwezo wa Mungu mimi nitakuwa salama na kama nitaendelea hivi, basi naweza kuwahi hata mchezo wetu na Sevilla endapo mwalimu atanipanga,” alisema.

Ziara ya Sevilla ambao ni mabingwa mara tano michuano ya UEFA Europa League na ikishiriki Ligi Kuu Hispania maarufu La Liga, inaratibiwa na SportPesa Tanzania na watacheza na Simba Mei 23, mwaka huu Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 

The post Wawa: Nitaiwahi mechi ya Sevilla appeared first on KWATA UNIT SPORTS & ENTERTAINMENT.



Post a Comment

0 Comments