

Amekuwa akiaminika kiasi Simba iliyoishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kupewa nafasi ya kucheza na Mbeligiji Patrick Aussems.
Dogo mwingine aliyeonja utamu wa mashindano ya kimataifa ni Enock Atta wa Azam ambaye alikichezea kikosi cha timu yake ya taifa ya Ghana katika fainali za Afrika kwa vijana U-20 kule Niger.
Kwa jumla kuna nyota wanane matata chipukizi waliotesa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, japo bahati ya mtende imemuangukia Rashid aliyetwaa ubingwa wa igi akiwa na Simba.
FEISAL SALUM- YANGA
Tangu amejiunga na Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amekuwa muhimu kwenye kikosi hicho ambapo amekuwa akitumiwa na Mwinyi Zahera kama kiungo mkabaji. Fei Toto, aliyezaliwa Januari 11, 1998 ni miongoni mwa wachezaji ambao wameitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars ambacho kitaingia kambini kujiandaa na Fainali za Mataifa ya Afrika Misri. Katika Ligi ya msimu huu licha ya kuwa miongoni mwa wachezaji waliolamba kadi nyingi za njano akipewa 10, lakini ameifungua Yanga mabao manne.
RASHID JUMA- SIMBA
Hajawa na nafasi ya kuanza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza cha Simba, lakini ni kinda aliyepata nafasi zaidi ya kucheza katika timu hiyo, kuliko hata Adam Salamba.
Rashid (21), amekuwa akitumika kama winga wa kushoto au kulia, amekuwa akiingizwa muda mwingine kujaribu kubadilisha matokeo hasa pale ambapo Haruna Niyonzima na Clatous Chama wanapodhibitiwa.
ABDALLAH SHAIBU ‘NINJA’- YANGA
Ana umri wa miaka 21, lakini tayari ameshapewa majukumu mazito ya kurithi mikoba ya Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye alistaafu msimu uliopita na kupewa jezi yake.
Amekuwa msaada kwenye safu ya ulinzi ya Yanga msimu huu hasa walipokuwa akiandamwa na majeraha, Andrew Vicent ‘Dante’ ambaye amezoeleka kuonekana akicheza na Kelvin Yondan.
Muda mwingine Ninja alikuwa akitumika na Zahera kucheza kama kiungo mkabaji akiwa na Feisal Salum kwa lengo la kuifanya Yanga kuwa imara zaidi kwenye safu ya ulinzi.
ALLY ALLY-KMC
Ubora wa KMC msimu huu hasa kwenye eneo lao la ulinzi, umechangiwa na kiwango cha Ally Ally ambaye alizaliwa Novemba 21,1999. Beki huyo naye ni miongoni mwa wachezaji ambao wameitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars.
ENOCK ATTA- AZAM
Azam ina machaguo mengi kwenye maeneo ya mawinga, Enock Atta ni kati ya mastaa wa timu hiyo ambao wanatoa wigo mpana kwa Meja Mstaafu wa Jeshi, Abdul Mingange.
Atta anayevalia jezi namba 10 amekuwa akifanya vizuri licha ya kuwa na umri mdogo, winga huyo ana umri wa miaka 20.
JONATHAN NAHIMANA-KMC
Lango la KMC ni wazi lipo kwenye mikono salama ya kinda Jonathan Nahimana kutoka Burundi mwenye umri wa miaka 20, pamoja na udogo wake ameweza kumpokonya namba mkongwe Juma Kaseja.
ISMAIL AIDAN- MTIBWA SUGAR
Mtibwa Sugar ambayo miaka nenda, rudi imekuwa kama kiwanda cha kuzalisha wachezaji kwa sasa miongoni mwa wachezaji wanojivunia kwenye kikosi chake ni Ismail Idan (20) ambaye amekuwa akicheza nafasi ya kiungo.
ISRAEL PATRICK- ALLIANCE
Huyu ni beki wa kushoto ambaye amekuwa akicheza kisasa kwa maana ya kupanda na kushuka ambaye amekuwa akifanya vizuri kwenye kikosi cha Alliance ya Mwanza tangu msimu uliopita.
Alikuwa sehemu ya kikosi cha Timu ya Taifa chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ , miaka mitatu nyuma ambacho kilishiriki fainali za Mataifa ya Afrika ‘Afcon U-17’ kwa mara ya kwanza kule Gabon.




0 Comments