

Ni msimu uliokuwa na matukio mengi ya kusisimua ambayo yanaacha kumbukumbu nzuri lakini pia kuna ambayo yanaacha kumbukumbu isiyovutia kutokana na namna yalivyokuwa na taswira ya tofauti.
Kwa wachezaji, kuna walionyesha kiwango bora na kutamba katika sehemu kubwa ya msimu lakini pia kuna waliochemsha na kushindwa kuzipa msaada timu zao na pengine watakuwa wanasubiria kipindi cha maandalizi ya msimu mpya, wajifue ili yale yaliyotokea msimu huu yasijirudie tena msimu ujao.
Katika kundi la wachezaji waliofanya vizuri, kuna wale ambao walifanya vizuri zaidi na hapana shaka walikonga nyoyo za wapenzi, mashabiki na wadau wa soka ambao wamekuwa wakifuatilia ligi hiyo.
Ingawa mtazamo wa makala haya haumaanishi kwamba wahusika ndio watatangazwa na kamati ya utoaji tuzo ya Ligi Kuu kama wachezaji bora wa msimu, ifuatayo ni tathmini ya wachezaji 11 ambao wanastahili kuunda kikosi bora cha Ligi Kuu msimu huu.
1. AISHI MANULA- SIMBA
Haukuwa msimu mzuri kwa idadi kubwa ya makipa wa timu za Ligi Kuu, kwani wengi wao hawakuonyesha viwango bora kwa kuokoa mashambulizi ya timu pinzani ambayo yalionekana kuwa yanaweza kuwa mabao lakini pia walikuwa wakifanya makosa ya kizembe ambayo yaliziponza timu zao na kuwapatia wapinzani mabao.
Pamoja na hilo, kipa wa Simba, Aishi Manula alijitahidi kuonyesha kiwango bora kwa kulilinda lango la timu yake kwa kuokoa mashambulizi ya ana kwa ana, kuipanga na kuikumbusha timu pamoja na kucheza mipira ya krosi na kona na hilo limemfanya awe kipa aliyefungwa idadi ndogo ya mabao akiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 14 tu.
2. PAUL GODFREY ‘BOXER’- YANGA
Msimu huu ndio kinda huyo aliyepandishwa kutoka kikosi cha vijana wenye umri chini ya miaka 20 cha Yanga, ambao ameutumia vyema kujihakikishia nafasi ya kudumu kikosini.
Uwezo wake katika kuwadhibiti washambuliaji wa timu pinzani pamoja na ule wa kupandisha mashambulizi umemfanya awe lulu kwenye kikosi cha Yanga na kufanikiwa kumpora namba mkongwe, Juma Abdul.
3. BRUCE KANGWA- AZAM
Beki wa pembeni anayekupatia kila unachokihitaji kwa mchezaji wa nafasi yake kukifanya.
Anacheza kwa nidhamu kubwa. Anashambulia na kuzuia kwa wakati sahihi na ni fundi wa kupiga krosi ambazo zimekuwa mwiba kwa mabeki wa timu pinzani.
4. ABDALLAH SHAIBU ‘NINJA’ -YANGA
Katika msimu ambao Kelvin Yondani hakuwa anacheza mara kwa mara huku Andrew Vincent ‘Dante’ akikumbwa na majeraha ambayo yalimpunguzia ufanisi ndani ya uwanja, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ aligeuka kuwa mhimili imara wa Yanga katika eneo la beki wa kati kutokana na uwezo wake wa kuwadhibiti washambuliaji wa timu pinzani akitumia vyema umbo lake kubwa na kila alipokosekana, Yanga ilikuwa na wakati kwenye safu ya ulinzi.
5. ERASTO NYONI-SIMBA
Utulivu wake wa hali ya juu na matumizi ya akili aliyonayo vilikuwa chachu ya kuifanya safu ya ulinzi ya Simba iwe imara msimu huu na kuifanya iruhusu idadi ndogo zaidi ya mabao kuliko timu nyingine na amekuwa chaguo la kwanza katika nafasi ya beki wa kati huku wenzake Pascal Wawa, Yusuph Mlipili na Juuko Murshid wakicheza kwa kupishana.
6. ALLY MSENGI-KMC
Ni zao la timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, Serengeti Boys akiwa mmoja wa nyota wa kikosi hicho kilichoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika huko Gabon kwa vijana wenye umri huo (AFCON U17) mwaka 2017.
Anacheza kwa nidhamu kubwa kwenye eneo la ulinzi licha ya umri wake mdogo wa miaka 19. Kazi kubwa aliyoifanya katika kutibua mashambulizi na mipango ya timu pinzani, kuchezesha timu na kupora mipira, imechangia kwa kiasi kikubwa kuifanya KMC kutikisa msimu huu.
7. DICKSON AMBUNDO- ALLIANCE
Sio kazi rahisi kwa mchezaji anayecheza nafasi ya winga au kushambulia kutokea pembeni kutikisa nyavu za timu pinzani kwa sababu muda mwingi anakuwa mbali na lango lakini hali iko tofauti kwa Dickson Ambundo ambaye mbali na uwezo wake wa kutengeneza nafasi, kupiga krosi na kupiga pasi za mwisho, pia ni mfungaji mzuri wa mabao ambapo kabla ya mechi za mwisho za Ligi Kuu tayari alishafunga mabao 10.
8. PAPY KABAMBA TSHISHIMBI-YANGA
Msimu uliopita alichezeshwa kama kiungo mkabaji lakini safari hii ametumika kama kiungo mshambuliaji nafasi ambayo ameicheza vyema kwa kutengeneza nafasi na kufunga mabao huku akitengeneza balansi ya kitimu ndani ya uwanja.
Katika Ligi Kuu amepachika mabao manne.
9. MEDDIE KAGERE- SIMBA
Mpira ni mabao na kama timu inayofunga idadi kubwa ya mabao ndio huwa na nafasi kubwa ya kuibuka bingwa wa mashindano husika na hilo linajidhihirisha kwa Simba ambayo imefunga idadi kubwa ya mabao msimu.
Na unapozungumzia makali ya Simba katika kufumania nyavu, basi hakuna namna unavyoweza kutomtaja mshambuliaji Meddie Kagere ambaye ameifungia timu hiyo zaidi ya 30% ya mabao yote iliyofunga msimu huu, akiibuka mfungaji bora na mabao yake 23.
10. HERITIER MAKAMBO-YANGA
Hakuonekana kama mshambuliaji tishio wakati alipotua Yanga lakini amegeuka kuwa tegemeo la klabu hiyo kwa kupachika mabao muhimu ambayo yameisaidia kupata pointi ambazo zimeifanya imalize kwenye nafasi ya pili.
Makambo ni mtaalamu hasa wa kutumia vyema nafasi anazopata ndani ya eneo la hatari la timu pinzani hasa kufunga mabao ya vichwa na pengine hilo ndilo limeishawishi klabu ya Horoya ya Guinea kumnunua kwa kiasi cha Dola 100,000 (zaidi ya Shilingi 230 milioni).
11. IBRAHIM AJIBU-YANGA
Namba huwa hazidanganyi na hilo unaweza kuliona kwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu ambaye kama ilivyo kwa Makambo, ametoa mchango mkubwa kwa timu hiyo msimu huu akiiifungia mabao sita na kutoa pasi 16 za mabao ambazo ni idadi kubwa kuliko mchezaji mwingine yeyote kwenye Ligi Kuu.
KOCHA ZAHERA-YANGA
Ni kweli Simba imebeba taji mbele ya Yanga, lakini hakuna ubishi Kocha Mwinyi Zahera amejitiofautisha na makocha wengine katika msimu huu. Akiwa na kikosi finyu na chenye matatizo lukuki, ameitengeneza Yanga yenye kutetemesha katika Ligi Kuu.
Kwa namna alivyoweza kuiongoza Yanga na kukaa kileleni kwa muda mrefu anastahili kabisa kukiongoza kikosi cha msimu akisaidiana na Patrick Aussems wa Simba.
WACHEZAJI WA AKIBA
Ayoub Lyanga wa Coastal Union anastahili kuwepo katika kikosi hiki, Pascal Wawa wa Simba, Aaron Kalambo wa Prisons, Salim Aiyee wa Mwadui, Nicholas Wadada na Mudathir Yahya wanastahili kuwepo katika kikosi cha akiba cha msimu huu.




0 Comments