Windows

JICHO LA MWEWE : Yanga wanavyoisumbua Simba huko Instagram na Facebook

MAISHA ya siku hizi bwana. Yana raha yake sana. Yamehama mitaani yamehamia katika simu. Ukiwa na simu unapata kila unachokitaka. Hakikisha haukosi bando lako la kufaidi kila tukio. Presha kubwa ya maisha imehamia Instagram na Facebook.
Ulikuwa msimu wa tabu kwa Yanga. Simba imechukua ubingwa kiulani. Yanga ilikuwa haina raha licha ya kuongoza ubingwa kwa muda mrefu. Simba imekula viporo vyake vyote kwa amani kabisa. Ilitabirika kwamba ingechukua ubingwa.
Yanga ilikuwa na matatizo mengi kabla ya kupata uongozi mpya. Wachezaji waligoma mara kadhaa baada ya kukosa mishahara. Timu ilisafiri kwa tabu. Kocha aligeuka kuwa mwenyekiti na mweka hazina wa timu, ulikuwa msimu wa tabu kwa Yanga. Unashangaa kwanini timu kama Azam na Mtibwa zilihenyeshwa na Yanga.
Kilichonichekesha ni hiki hapa. Tangu msimu uliopita Yanga imejua namna ya kutibua sherehe za ubingwa kijanja. Wamehamia mitandaoni na kutafuta fursa za kusahau matatizo yao na kujiliwaza kwa mapungufu machache ya Simba.
Kwa mfano, msimu uliopita Simba ilitamba ikachukua ubingwa wake. Nusura ichukue ubingwa bila ya kupoteza mechi. Ikapoteza mechi siku ya mwisho ya msimu ilipofungwa na Kagera Sugar bao 1-0 Uwanja wa Taifa mbele ya macho ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, John Pombe Magufuli.
Yanga hawakupoteza fursa hiyo. Badala ya kujikumbusha kwamba walikuwa na msimu mbovu wao wakawa bize kushangilia kichapo cha Simba dhidi ya Kagera katika siku ya mwisho. Na hasa pale Rais aliposema ‘Simba wametobolewa tundu’.
Msimu huu Yanga wameendeleza tabia ileile. Tazama jinsi tajiri wa Simba, Mohamed Dewji alipojichanganya na kuamua kuwazawadia wachezaji wake pikipiki. Kwangu ni udhaifu. Baada ya Simba kuchukua ubingwa wa Bara, huku ikifika robo fainali ya Ligi ya mabingwa wa Afrika, ni kweli wanachostahili wachezaji wa Simba ni bodaboda?
Ghafla watu wa Yanga wakasahau matatizo yao yote na kuanza kuwahenyesha Simba mitandaoni, hasa Instagram. Yanga wamesahau kwamba huu ni moja kati ya misimu michache katika historia yao ambapo wameruhusu kufungwa mechi tatu mfululizo.
Badala ya kujadili udhaifu wao wakavamia habari ya bodaboda kule Instagram. Nilitazama sura ya watu wa Simba nikaona wazi hawana raha na habari hii. Imewatibulia raha zote za ubingwa. Sijui huwa wanakosea wapi.
Baada ya hapo Yanga wakaendelea kujificha katika masuala ya Simba. Safari hii sio udhaifu. Picha za marudio zilikuwa zinawaonyesha wachezaji wa Simba wakibadilishana jezi, gloves na viatu na wachezaji wa Sevilla ya Hispania.
Habari ya Adam Salamba kuchukua kiatu kwa Ever Benega ikawa kubwa zaidi. Yanga wakaitumia kama kejeli mitandaoni kuwanyamazisha Simba. Ulikuwa ni ujanja ujanja tu wa Yanga kuhakikisha Simba hawazungumzii mabao yao manne waliyofunga katika nyavu za Sevilla.
Sawa, Simba ilifungwa 5-4, sawa muda mwingi Sevilla walionekana kucheza kama Villa Squad. Wachezaji wao hawakutaka kukimbia. Kiakili walikuwa wameshaanza likizo zao wakati wamekuja nchini. Lakini, sio mbaya kukumbusha kwamba wachezaji wa Simba, hasa washambuliaji, walimuonyesha Kocha wa Sevilla, Joaquín Caparrós kama wangeandaliwa mapema wangetamba Ulaya.
Yanga walitaka kuziba mdomo kelele za Simba kuhusu mabao yao manne kwa kuzungumzia zaidi viatu alivyopewa Salamba na Banega. Huu ndio ujanja ujanja ambao Yanga wameishi nao kwa msimu miwili hii. Unashangaa nini sasa.
Ni wazi ilikuwa misimu miwili mibovu kwa Yanga. Ni wazi Yanga wamepitia katika aibu kubwa ndani ya misimu hii miwili. Haikudhaniwa katika zama kama hizi wangerudi katika bakuli. Hata hivyo, waliamua kujifariji katika dunia ya mitandao.
Ukweli utabakia palepale Simba wako hatua nyingi sana mbele ya Yanga. Kama Yanga hawatajirekebisha kupitia kwa uongozi mpya, tunaweza kuanza kuona mechi mbovu zaidi za wapinzani wa jadi kama ile ya raundi ya kwanza ya msimu huu. Na pia tunaweza kuona msimamo wa ligi unaotabirika zaidi kama tulivyoona jinsi ambavyo msimu huu Yanga walikuwa wanaongoza ligi lakini Simba ilikuwa inajulikana inakuja kuchukua ubingwa.
Yanga inabidi wapambane. Tabia ya kwenda Instagram kuwa bize na mapungufu machache ya Simba kuliko mwelekeo wa timu yao nadhani inabidi ifike mwisho. Sawa, wanachofanya ni utani lakini pengo baina ya mabosi hawa wawili wa Kariakoo limezidi kuwa kubwa ndani ya misimu hii miwili.
Naona mikwara yao katika magazeti wakishusha vifaa vya kupambana na Simba na Azam FC msimu ujao. Viwe vifaa kweli. Vinginevyo wataendelea na kazi ileile waliyoifanya katika misimu miwili iliyopita. Kazi ya kusubiri Simba wachukue ubingwa huku wakisubiri wateleze katika mambo ya kawaida na wao wayakuze kuliko hali ilivyo kwao. Kila la kheri kwao.

Post a Comment

0 Comments