


KUTUA nchini kwa nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Samatta, kunanogesha maandalizi ya timu hiyo itakayopiga kambi kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Mataifa ya Afrika mwaka huu.
Samatta ataungana na wachezaji wengine wa kimataifa ambao tayari wameshatua nchini kwa ajili ya michuano hiyo inayotarajiwa kutimua vumbi Juni 21 hadi Julai 19, mwaka huu nchini Misri.
Akizungumza na BINGWA jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, alisema kambi ya timu hiyo huenda ikaanza Juni mosi mwaka huu baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara kesho.
“Samatta na wachezaji wengine tayari wamewasili, lakini hawawezi kuingia sasa kambini mpaka ligi imalizike, hivyo kambi inaweza kuwa Juni mosi au mbele kidogo,” alisema Ndimbo.
Katika kujiandaa na michuano hiyo ya Afcon 2019, Stars itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Misri, ambapo mchezo huo umepangwa kufanyika Juni 13, mwaka huu kwenye Uwanja wa Borg El Arab, Cairo.
Stars imepangwa Kundi C katika michuano hiyo pamoja na timu kama Senegal, Algeria na Kenya.



0 Comments