Windows

Wachezaji Yanga 'wamvulia kofia' Zahera



Moja ya mafanikio ya Yanga msimu huu ni kuipa presha Simba iliyokuwa imekamilika kila idara huku ikinuka fedha za 'Mo' na kufanya hatma ya ubingwa kuamuliwa mwishoni mwa msimu

Wakati ligi ikianza hakuna aliyeamini kama Yanga ingeweza kushindana na timu za Simba na Azam Fc kutokana na ukweli kuwa hali ya kiuchumi ya Yanga ilikuwa mbaya sana

Lakini ukiwauliza wachezaji wa Yanga leo ilikuwaje mpaka wakaweza kupambana licha ya timu kukabiliwa na changamoto nyingi, watakwambia kocha Mkuu wa timu hiyo Mwinyi Zahera ndiye 'sterling'

Licha ya kutimiza majukumu yake ya ukocha, nje ya uwanja Zahera alikuwa kiongozi na mhamasishaji namba moja

Alitumia muda mwingi kuwaandaa wachezaji wake kisaikolojia kabla ya mchezo na hata pale mambo ya fedha yalipokwenda kombo, alichukua wajibu kama mzazi na kuwasaidia wachezaji shida zao

Kuna wakati Zahera alitoa fedha zake mwenyewe kuwapa 'bonus' wachezaji kila baada ya mchezo

Nahodha Msaidizi wa Yanga Juma Abdul juzi katika hafla ya Iftar Dinner iliyofanyika Hoteli ya Serena Jumamosi, alitambua mchango wa Zahera na kuutaka uongozi wa Yanga kuhakikisha kocha huyo haendi popotecut

"Kwa kweli kwanza tunaomba viongozi wetu wasimruhusu mwalimu Zahera aondoke, huyu jamaa ninaamini ana kitu kikubwa zaidi cha kutufanyia hapo mwakani, kwani msimu huu amepambana vya kutosha kuhakikisha Yanga inapata heshima yake," alisema Abdul


Lakini sio Abdul pekee aliyeona maajabu ya Zahera, wachezaji karibu wote wa Yanga wameikubali kazi ya Zahera wakiamini uwepo wake Jangwani utaifanya timu hiyo iwe moto wa kuotea mbali msimu ujao

Tambwe : "Kama kuna mtu ambaye anahitaji pongezi Yanga ni Zahera, kwani amepambana kutujenga kisaikolojia na kutuusia kiasi kikubwa kimawazo kuhakikisha tunapata matokeo uwanjani,"


"Huyu jamaa ni mkali sana na hana mchezo katika kazi yake hasa pale tunapokuwa tunahitaji kushinda, kwa kweli amepambana sana kwani tulikuwa tumeshakata tamaa kila mmoja alikuwa anawaza lake"


Yondani : Sina kinyongo na Zahera licha ya kunivua kitambaa cha unahodha na kumpa Ajib, kwani hiyo yote ilitokana na msimamo wake katika kujenga nidhamu"

“Jamaa noma, kwa kweli kapambana na sisi hatukutaka kumwangusha, mwakani tutafanya vizuri zaidi kuliko mwaka huu’’

Boban : "Zahera ni bonge la kocha, kwani ushawishi wake ulichangia mimi kujiunga na Yanga katika kipindi cha dirisha dogo"

“Ni kocha mzuri, mengine tuombe uzima, mwakani tutajitahidi kufanya vizuri na kuchukua ubingwa"


Uongozi wa Yanga umeahidi kumpatia Zahera zote za usajili alizohitaji ili kukiimarisha kikosi cha timu hiyo

Mwenyewe ameahidi kuwa msimu ujao lengo la kwanza la Yanga ni kutwaa ubingwa wa ligi kuu na kombe la FA

Post a Comment

0 Comments