ZIKIWA zimebaki siku chache kabla Ligi Kuu Tanzania Bara kufikia tamati, wachezaji wa Yanga wamesema kama si Kocha Mkuu wao, Mwinyi Zahera, timu hiyo ingeshuka daraja msimu huu.
Nyota hao walitoa kauli hiyo katika hafla ya futari iliyoandaliwa na viongozi wa timu hiyo iliyofanyika juzi katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau kibao wa soka hapa nchini na Wanayanga.
Wakizungumza nasi katika tukio hilo, wachezaji Kelvin Yondani, Juma Abdul, Haruna Moshi ‘Boban’ na Amissi Tambwe, walisema Zahera si mtu wa mchezo mchezo anapohitaji jambo lake litimie.
Beki Juma Abdul ambaye ni nahodha msaidizi alisema Zahera ni mtu, kwani kama si msimamo wake timu hiyo mapema ingeshuka daraja msimu huu kwa jinsi ilivyokuwa na hali mbaya ya kiuchumi.
“Kwa kweli kwanza tunaomba viongozi wetu wasimruhusu mwalimu Zahera aondoke, huyu jamaa ninaamini ana kitu kikubwa zaidi cha kutufanyia hapo mwakani, kwani msimu huu amepambana vya kutosha kuhakikisha Yanga inapata heshima yake,’’ alisema Abdul.
Kwa upande wake, Tambwe alisema kama kuna mtu ambaye anahitaji pongezi Yanga ni Zahera, kwani amepambana kuwajenga kisaikolojia na kuwausia kiasi kikubwa kimawazo kuhakikisha wanapata matokeo uwanjani.
“Huyu jamaa ni mkali sana na hana mchezo katika kazi yake hasa pale tunapokuwa tunahitaji kushinda, kwa kweli amepambana sana kwani tulikuwa tumeshakata tamaa kila mmoja alikuwa anawaza lake,’’ alisema Tambwe.
Naye Yondani alisema hana kinyongo na kocha huyo licha ya kumvua kitambaa cha unahodha na kumpa Ibrahimu Ajib, kwani hiyo yote ilitokana na msimamo wa kocha huyo katika kuwajenga kinidhamu.
“Jamaa noma, kwa kweli kapambana na sisi hatukutaka kumwangusha, mwakani tutafanya vizuri zaidi kuliko mwaka huu,’’ alisisitiza Yondani.
Boban naye hakuwa nyuma kummwagia sifa kocha huyo, akisema Zahera ni bonge la kocha, kwani ushawishi wake ulichangia yeye kujiunga na Yanga katika kipindi cha dirisha dogo.
“Ni kocha mzuri, mengine tuombe uzima, mwakani tutajitahidi kufanya vizuri na kuchukua ubingwa,’’ alisema Boban.
0 Comments