KESHO uwanja wa Uhuru utakuwa na kazi ya kuhimili miguu 22 ya wanaume wenye hasira ambao watakuwa kazini kutafuta pointi tatu muhimu.
Simba itaikaribisha Azam FC kwenye mchezo huo ambao utavuta hisia za mashabiki kutokana na ushindani uliopo kwa vigogo hao wa soka nchini.
Mchezo wa kwanza, Azam FC walipoteza kwa kufungwa mabao 3-1 uwanja wa Taifa hivyo kesho ushindani unatarajiwa kuwa mkali zaidi kwa timu zote.
Matokeo ya timu zote mbili kwenye michezo yao ya mwisho karibuni hayajawa chanya kwao kutokana na namna ambvyo dakika 90 ziliwaendea mrama kwani hakuna aliyepata bahati ya kusepa na pointi tatu.
Azam FC wao mchezo wa mwisho wakiwa nyumbani walitoka suluhu na KMC uwanja wa Chamazi na kuwafanya wagawane pointi moja moja.
Simba wao walionja joto ya jiwe baada ya kutoa zawadi ya bao kwa Kagera Sugar kupitia kwa Mohamed Hussein na kupeleka pointi zote tatu Kagera Sugar.
Simba ipo nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 81 imecheza michezo 32 huku wapinzani wao Azam FC wamecheza michezo 35 wana pointi 68 kibindoni.
0 Comments