


STRAIKA wa Yanga mwenye uwezo mkubwa wa kupiga vichwa na kufunga mithili ya nyoka hatari Cobra, Amis Tambwe, amefunguka na kuweka wazi kuwa hatima ya kuongeza mkataba katika timu hiyo ipo mikononi mwa kocha Mwinyi Zahera.
Tambwe alitoa kauli hiyo kutokana na mkataba wake na timu hiyo ambayo ameichezea kwa mafanikio makubwa tangu ajiunge nayo msimu wa mwaka 2014 kumalizika.
Akizungumza na BINGWA jana, Tambwe alisema amekuwa katika kiwango bora siku zote tangu ajiunge na mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara na ana imani kuwa mambo yatakuwa mazuri kama atatakiwa kuwepo ndani ya kikosi hicho.
“Sijajua bado hatima yangu kama nitaongeza au vipi yote kwa yote kocha Zahera (Mwinyi), yeye ndio anajua kama bado atanihitaji au vipi, siwezi kujipa asilimia mia moja,’’ alisema Tambwe.
Itakumbukwa kuwa Tambwe ndio mchezaji pekee wa Yanga aliyeweka rekodi ya kutengeneza nafasi tatu za mabao na kufunga mabao matatu kwenye msimu wa mwaka 2015.
Mbali na rekodi hiyo, lakini pia Tambwe amekuwa ndio mshambuliaji wa kwanza kupiga ‘hat-trick’ katika mechi tatu tofauti kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Mrundi huyo, ni mchezaji pekee aliyeweka rekodi hiyo ambayo haijawahi kuwekwa na mchezaji yeyote tangu uwanja huo ulipoanza kutumika.
Mechi yake ya kwanza kufunga ‘hat trick’ kwenye uwanja huo ilikuwa ni Februari mosi, 2014 dhidi ya JKT Oljoro akiwa na Simba ambayo ilishinda 4-0.
Mechi nyingine ambayo straika huyo alifunga ‘hat trick’ ilikuwa ni Septemba 19, 2014 dhidi ya Mgambo JKT, ambayo timu yake ya Simba ilipata ushindi mnono wa mabao 6-0.
Mshambuliaji huyo alikamilisha rekodi yake ya kupiga ‘hat-trick’ msimu wa 2015 wakati akiwa na Yanga na kufunga mabao manne katika ushindi wa mabao 8-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga.



0 Comments