DIRISHA la usajili likifunguliwa, Yanga huenda ikafanya kazi moja tu kutangaza orodha ya kikosi chake na watakapopiga kambi.
Kama mambo yakienda sawa huenda kabla ya Ligi haijamalizika wakatangaza kabisa wanaoachwa bila kupepesa macho. Kocha Mwinyi Zahera amemalizana na kiungo mshambuliaji wa Kati wa Kariobang Sharks ya Kenya, Duke Abuya.
Mchezaji huyo mwenye umbo kubwa na machachari amemwaga wino kwenye mkataba wa miaka miwili mbele ya Mwinyi Zahera.
Abuya aliichapa Yanga mabao mawili katika mchezo wa robo fainali ya Mashindano ya SportPesa ambapo Wakenya hao walishinda mabao 3-2 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Januari 22, mwaka huu.
Chanzo makini kutoka ndani ya Yanga kimeeleza kuwa, tayari kocha wao Mwinyi Zahera ameshamalizana na kiungo huyo na kilichobaki ni kutua nchini kwa ajili ya kutambulishwa rasmi kwa mashabiki.
“Kocha ameshamalizana na kiungo mshambuliaji wa Kariobang Sharks ya Kenya, Duke Abuya ambaye ameingia mkataba wa miaka miwili na kwamba muda wowote mara baada ya ligi kukamilika atatua nchini kuitumikia klabu yetu.
“Huyu Abuya ni moja ya wachezaji wazuri ambao walitufunga katika mashindano ya Sportpesa,” kilisema chanzo chetu na kuongeza kuwa Mzimbabwe Rodrick Mutuma yupo Dar es Salaam kukamilisha mambo yake na Yanga.
Mutuma ni raia wa Zimbabwe anayeichezea FC Lupopo ya DR Congo na kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Mazembe aliwatungua bao 1-0.
Habari za ndani zinasema kwamba Zahera amepewa fungu na Kamati ya Uhamasishaji ya Yanga na anataka kumaliza usajili mapema kabla hajaenda kwenye fainali za Afcon mwezi ujao ambako anainoa DR Congo.
0 Comments