SASA ni uhakika wa asilimia 99 kwamba Simba ni bingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2018/19. Huu utakuwa ni ubingwa wa pili mfululizo kwa Wekundu wa Msimbazi ambao kwa miaka miwili sasa wanatawala soka la Tanzania.
Simba wamekuwa na uhakika wa ubingwa baada ya juzi Jumapili kuichapa Ndanda mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kufikisha pointi 88 wakibakiwa na michezo mitatu, huku wapinzani wao wa karibu, Yanga wakiwa na pointi 83 wakibakiwa na michezo miwili tu.
Hii maana yake ni kwamba Simba wanahitaji pointi moja tu kabla ya kutangaza ubingwa na wanaweza wakaipata pointi hiyo katika mechi ya leo Jumanne dhidi ya Singida United kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.
Wakipata pointi hiyo watafikisha pointi 89 ambazo ndizo Yanga wanaweza kuzifikisha kama wakishinda michezo yao miwili iliyobaki, lakini hawatafua dafu kwani baada ya timu kulingana pointi, kinachoangaliwa ni utofauti wa mabao, na Mnyama ana utofauti wa mabao 30 zaidi ya Yanga.
Ili Yanga wafikie tofauti hiyo, watatakiwa kushinda 15-0 katika kila mechi kwenye mechi mbili walizobakiza kitu ambacho hakiwezekani.
Mabao yote ya Simba juzi yalifungwa na mshambuliaji hatari Mnyarwanda, Meddie Kagere ambaye sasa amefikisha mabao 22 na kuvunja rekodi ya Amissi Tambwe iliyodumu kwa miezi 36 au siku 1105.
Tambwe akiwa Yanga alifunga mabao 21 msimu wa 2015-16, tangu hapo hakuna mfungaji mwingine aliyewahi kufikisha idadi hiyo, kabla ya Kagere kuifikia juzi. Tambwe msimu huo, alifunga bao lake la 21 katika ushindi wa 2-0 ugenini dhidi ya Mbeya City Mei 10, 2016, tangu hapo zimepita siku 1105 au miezi 36 kabla ya MK 14 kuvunja rekodi hiyo.
Kihistoria, straika wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Chinga One’ ambaye ni mchambuzi wa Championi, ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao mengi zaidi msimu mmoja Bongo alipofunga mabao 26 msimu wa 1998/99, anayefuata baada yake sasa ni Kagere (22) halafu Tambwe (21).
Katika mchezo wa juzi, Kagere alifunga bao la kwanza dakika ya 5 kwa shuti la mguu wa kushoto na akafunga la pili dakika ya 11. Simba wangeweza kufunga bao la tatu dakika ya 16 lakini John Bocco alikosa nafasi ya wazi akiunganisha krosi ya Haruna Niyonzima. Beki wa Ndanda aliokoa mpira ukiwa unaelekea wavuni.
Simba waliutawala mchezo wa juzi, na walikuwa na nafasi ya kupata mabao mengi. Licha ya Ndanda kufanya mabadiliko kadhaa kwa kumtoa Mohamed Mkopi na kumuingiza Yusuph Mhilu dk ya 56, na kumuingiza Salum Chubi badala ya Kigi Makasi dk ya 77, bado walizidiwa sana na Simba ambao walikuwa wakilishambulia lango la Ndanda kama nyuki karibu muda wote wa mchezo.
Simba wao walimtoa Hassan Dilunga dk ya 46 na kumuingiza James Kotei, kisha Rashid Juma akaingia badala ya John Bocco dk ya 82.
The post Simba Bingwa Asilimia 99 appeared first on Global Publishers.
0 Comments