MWANADADA wa Kitanzania, Angel Eaton, kwa mara ya kwanza amezungumza kuhusu magumu aliyopitia mpaka kutoboa na kufanikisha kunyakua jumla ya tuzo na makombe 34 ya mchezo wa GOLF ikiwemo tuzo ya hivi karibuni ya Ubingwa wa GOLF Afrika Mashariki na Kati ya mwaka 2019.
Angel ambaye kituo chake cha michezo kipo Lugalo jijini Dar es Salaam amefunguka hayo wakati akifanya kipindi maalum na Kituo cha 255 Global Radio, leo Jumanne, Mei 21, 2019 alipotembelea studio za radio hiyo.
“Nikiwa mdogo nilianza kucheza tennis na GOLF taratibu sana, mara ya kwanza sikuupenda kabisa huu mchezo, lakini nilipondelea nilijikuta nikizoea, nikaona kipaji changu hakipo kwenye tennis, hivyo nikahamia rasmi kwenye GOLF.
“Ili uweze kuumudu mchezo huo, kuna stages tatu, kwa wanawake huwa tunaanzia na hand cape 36, lakini wanaume wanaanzia hand cape 24, utaingia 18, kisha 12 na mwisho 0, baada ya hapo unakuwa professional.
“Kufikia stages hizi zote kwangu mimi ilichukua mwaka mzima kuuelewa vizuri mchezo, na hapo sio kupiga mipira kumi, unatakiwa angalau upige mipira 500 kwa siku, kwa hiyo haikuwa kazi rahisi,” alisema.
Amesema kwa sasa ana tuzo zipatazo 34 ambazo ameshinda katika mashindano mbalimbali ya kimataifa na ya ndani ikiwemo ya Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati aliyopata hivi karibuni huku akitaja kuwa siri ya mafanikio yake hayo ni kujituma katika mazoezi yake na kuondoa uoga.
Aidha, gazeti namba moja la michezo Tanzania, Championi linalochapishwa na Kampuni ya Global Publishers limemtunuku Angel, Tuzo ya Heshima kutokana na umahiri wake kwenye tasnia ya GOLF na kutambua mchango wake kwenye mchezo huo na namna anavyoiwakilisha nchi yetu kimataifa.
Akifungukia tuzo hiyo, Angel amesema: “Kwa kweli ni jambo kubwa sana katika maisha yangu ambalo Championi wamenifanyia leo, sijawahi kufanyiwa kitu kama hiki, sikuwahi kufikiria kama kitu hiki ningeweza kufanyiwa.
“Ninawashukuru sana Global Publishers na Global Radio kwa kutambua mchango wangu, hii imenipa hamasa kubwa na nguvu ya kuendelea kupambana zaidi, sasa ninajiona kama staa.”
Amesema iwapo akipata nafasi katika mashindano y Olympic ya mwakani yupo tayari kwenda kuiwakilisha nchi vizuri na anaamini kutokana na uwezo wake mkubwa wa kusakata GOLF, na sapoti ya Watanzania, atanyakua ushindi na kuipaisha Tanzania tena.
Akizungumzia changamoto katika mchezo huo, Angel amedai kuwa tatizo kubwa ni ubovu wa viwanja, miundombinu ya mchezo huo, vifaa vya michezo ambavyo ni bei ghali sana (set moja inagharimu zaidi ya Tsh milioni 3) hivyo watu wengi hushindwa kumudu kuvinunua.
Amebainisha jambo jingine linalokwamisha ukuaji wa mchezo huo hapa nchini ni ugumu wa kupata wadhamini.
VIDEO: MSIKIE ANGELA KIFUNGUKA
The post Huyu Ndo Mwanamke Mtanzania, Bingwa wa GOLF A. Mashariki Mwenye Tuzo 34 – Video appeared first on Global Publishers.
0 Comments